Wito umetolewa kwa uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe (MU) kuanzisha mfuko wa ufadhili wa wahitimu wa Chuo hicho “ Alumni Scholarship Scheme”.
Uazishwaji wa mfuko huo utawasaidia Watanzania ambao wana sifa ya kusoma katika ngazi ya Chuo Kikuu lakini kutokana na ukosefu wa fedha wanakosa hiyo fursa muhimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ametoa wito huo katika mkutano mkuu wa 22 wa Baraza la Masajili la Chuo Kikuu cha Mzumbe uliofanyika katika ukumbi wa Maekani uliopo Kampasi kuu ya Chuo hicho mkoani Morogoro.
Amesema mfuko huo utasaidia wanafunzi wanaongia chuoni na kushindwa kuendelea na masomo yao kutokana na ukosefu wa fedha.
Hemed ameeleza kuwa yenye ni mmoja kati ya waliosoma chuoni hapo na kusema uanzishwaji wa mfuko utasadifu kauli mbiu ya Chuo kikuu hicho inayosema “ Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”.
Amesema Chuo kikuu hicho ni kati ya Vyuo vikuu nchini vinavyofanya vizuri kwa kutoa viongozi wa ngazi ya juu ikiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na wengine waliopo serikalini na sekta binafsi.
Hemed pia ameushauri uongozi wa Chuo kuangalia namna ya kuanzisha ushirikiano na Vyuo vya Zanzibar ili kutanua wigo wa kuchagua Program za kujiufunza na kusogeza fursa ya elimu kwa Wazanzibari.