Home Elimu Dkt. Biteko ataka mitaala vyuoni iendane na mabadiliko ya teknolojia

Dkt. Biteko ataka mitaala vyuoni iendane na mabadiliko ya teknolojia

0 comment 8 views

Vyuo na taasisi zinazotoa elimu ngazi ya kati ikiwemo zimetakiwa kuboresha mitaala yake ya masomo ili iendane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira kimataifa sambamba na mahitaji ya kijamii na kiuchumi.

Hayo yamebainishwa Januari 21, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kilichoanzishwa Januari 21,1965.

“Serikali inasisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu za kujifunza zinazojibu changamoto za kimataifa,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema kuwa Serikali inazitaka taasisi za elimu ya kati ikiwemo CBE kuweka mkazo kwenye mafunzo ya ujasiriamali, ili wahitimu wake waweze kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa kupitia biashara bunifu na ajira binafsi.

Aidha, taasisi za elimu, zikiwemo vyuo kama CBE, amezitaka kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira na pia kusaidia kukuza sekta hiyo kwa utafiti na mafunzo.

Ameongeza kuwa, Serikali inahimiza vyuo vya elimu ya biashara kufanya tafiti za kina zinazosaidia kutatua changamoto za kiuchumi, kuimarisha sera za biashara, na kubuni suluhisho endelevu.

“Serikali imeelekeza  taasisi kama CBE zihakikishe kwamba fursa za elimu zinafikia makundi yote ya jamii, wakiwemo wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, ili kuongeza ushiriki wa makundi yote katika uchumi wa taifa, “ameeleza Dkt. Biteko.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara amesema  CBE ni kitovu cha biashara nchini na kimeweza kujenga mahusiano na nchi mbalimbali kimataifa ikiwemo nchi ya China na Ujerumani na ni ufunguo wa ufanyaji wa biashara katika kampasi zote nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema CBE imekuwa ikifanya kazi nzuri na kina mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta ya fedha hapa nchini.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.

“Vile vile, Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Edda Lwoga amesema kuwa katika maadhimisho ya miaka 60 ya CBE wemekuwa wakitoa elimu ya biashara kwa makundi mbalimbali ya kijamii na pia wametoa mafunzo ya muda mfupi kwa wadau mbalimbali.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter