Serikali ya Tanzania itaokoa Sh bilioni 500 ambazo zinatumika kununua mafuta, vipuri na kufanya matengenezo ya magari ya viongozi.
Fedha hizo zitaokolewa endapo serikali itawakopesha viongozi wenye hadhi ya kuwa na magari magari hayo na kuwa yao tofauti na sasa ambapo magari hayo yanamilikiwa na kufanyiwa matengenezo na serikali.
Akiwasilisha bajeti ya Fedha kwa mwaka 2022/23 Bungeni Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametoa mapendekezo ya kuwakopesha magari watumishi wenye hadhi ya kuwa na gari la Serikali.
Amesema “tukiwakopesha magari haya watasimamia vizuri matumizi ya mafuta, vipuri na magari yenyewe tofauti na hali ilivyo sasa.”
Waziri amebainisha kuwa kuna baadhi ya viongozi hutumia vibaya magari hayo pamoja na mafuta.
“Unakuta kiongozi anatoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, gari linakuja na dereva na yeye anapanda ndege,” amesema Dk Nchemba.
Ameeleza kuwa kwa sasa Serikali inatumia takribani Sh bilioni 550 kwa mwaka kwenye magari ambapo ikiwakopesha watumishi magari hayo itatumia Sh bilioni 50.5 na kuokoa Sh bilioni 500.
“Tumezidi mno kupenda uboss serikalini wakati kuna watu hata mlo mmoja hawana,” amesema Dk Nchemba akieleza kuwa fedha hizo zitaweza kutumika kununua madawa na kutoa mikopo kwa vyuo vya kati.
Katika bajeti hiyo, Waziri Nchemba amezungumzia suala la ulipaji kodi na maduhuli ya serikali akionya rushwa kwa wafanyabiashara na watoza kodi.
Ameeleza kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu imedhamiria kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara.
Kwenye sekta ya elimu, Waziri Nchemba alipendekeza kufutwa kwa ada ya kidato cha tano na sita.
Amesema Serikali itajipanga kusaidida vyuo vya kati kadri hali ya uchumi itakavyokuwa.