Home Elimu Serikali yawataka wahitimu kuwa waadilifu kazini

Serikali yawataka wahitimu kuwa waadilifu kazini

0 comment 156 views

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wahitimu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI)kutumia elimu waliyoipata kuwa waadilifu, wazalendo, kusimamia uhifadhi pamoja na matumizi endelevu ya misitu.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti, Dkt. Edward Kohi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas wakati wa mahafali ya 26 ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi ambapo ametunuku wanafunzi 200.

Kati ya hao, 124 ni wa Astashahada na 76 wa Stashahada za Teknolojia ya Viwanda vya Misitu za Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi.

” Nawaasa Wahitimu mnaohitimu leo kutumia elimu mliyoipata kuwa waadilifu, wazalendo na kuheshimu dhamana mtakayopewa katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu,” amesema.

Dkt. Kohi ameongeza kuwa “wahitimu wana mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa misitu na mazingira zinazoongezeka kwa kasi hapa nchini, ni wajibu wenu kutumia elimu na mbinu mlizozipata na kuwa wabunifu katika kutoa huduma kwa wananchi kwa bidii na haki”.

Amesema wahitimu wa fani ya teknolojia ya viwanda vya misitu ni hazina kubwa kwa Taifa ikizingatiwa kuwa ndiyo wanaohitajika zaidi kwa matumizi endelevu ya maliasili za misitu nchini kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Mafunzo haya ni muhimu sana katika jitihada za Serikali za kukuza uchumi na kuondoa umaskini.”amesema

Ameeleza kuwa Taifa linahitaji wahitimu wenye ujuzi wakutosha na nidhamu kwa matumizi endelevu ya misitu na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo yenye ubora katika sekta ya misitu na nyuki ili kujenga uchumi imara na kukuza ajira kwa vijana.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kuimarisha mfumo mzuri wa kuwapatia nafasi za kazi vijana kila fursa zitakapopatikana.

Aidha, ameutaka Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kukisaidia Chuo hicho ili kujenga uzoefu na kutumia wanafunzi wa chuo hiki katika kazi za kuendeleza na kuhamasisha matumizi ya misitu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter