Si kila anayefanya shughuli fulani huwa na utaalamu nayo,wengine wanaifanya kwa kuwa tu nafasi ilitokea ya kuifanya.
Na hautachukua muda kumgundua mtu anayefanya kazi zake kwa utaalamu,na yule anayebangaiza njaa tu,kwa jinsi wanavyoenenda na tabia zao.
Mara nyingi waajiri na wateja hulalamika kuwa anayewafanyia kazi hana utaalamu.
Yawezekana humalizi kazi vizuri, umemcheleweshea au hata kumzungusha kwa muda mrefu bila taarifa sahihi.Si mara moja tunasikia ni jinsi gani tunatakiwa kuwa wataalamu katika shughuli tunazofanya.
Kama unataka kupata mafanikio,kuchukuliwa kama mtu makini, kuonekana una mchango kwa unaofanya nao shuguli zako,kuzifanya kitaalamu ndio njia pekee ya kukufikisha huko.
Lakini tujiulize waajiri/wateja wanatafsiri gani juu ya utaalamu?
Wengi wao watakuona mtaalamu ikiwa wewe:
*Unafika eneo la kazi katika muda unaotakiwa;
*Unaifanya kazi uliyopewa vizuri;
*Unamaliza kazi kwa wakati.
Unadhani kuna matukio mengine ambayo unahisi ukiyafanya yatakuonyesha wewe si mtaalamu?
Kuna matukio ukiwa unayafanya yanakutafsiri moja kwa moja kuwa wewe si mtaalamu wa shughuli unayofanya,kwa mfano ukiwa:
*Unachelewesha kazi za watu;
*Unahudhuria vikao ukiwa haujajiandaa;
*Unatumia muda mwingi kuongea umbea muda wa kazi;
*Wavunjia heshima wenzako;
*Wasubirisha wateja muda mrefu bila sababu za msingi;
*Unaiba mawazo ya watu wengine kufanyia shughuli zako bila kuwahusisha;
*Vunja ahadi zako mara kwa mara.
Hebu leo tuangalie njia kumi utakazoweza kutumia kuwa mtaalamu katika shughuli yoyote unayofanya:
Jitahidi kufanya shughuli zako kitaalamu na watu waweze kukuamini, kukuheshimu, na kukuona una uwezo wa kipekee.Japo mazingira ya kila kazi yanatofautiana lakini linapokuja suala la utaalamu huwa na tafsiri moja dunia nzima.
Hebu tuangalie sifa za kuwa mtaalamu ni zipi:
1.UMAHIRI:
Lazima uwe mahiri katika kile unachofanya,ukitumia ujuzi na maarifa ya kutosha katika kazi yako lazima utaonekana mtaalamu na watu.
2.ZINGATIA MUDA:
Watu watakuwa wanakutegemea wewe ufike katika muda unaotakiwa ili shughuli ziende na umalize kwa wakati.Sio kuendelea kufanya shughuli zako kwa mazoea tu bila kujali muda,kwani hakuna anayependa kumuamini na kumpa kazi mtu asiyemaliza kwa wakati.
3.UAMINIFU:
Unatakiwa kuwa muwazi wa shughuli zako,na wale unaofanya au unaowafanyia kazi nao wajue nini kinachoendelea.Ukianza kujifanya mjanja mjanja, katika shughuli unayofanya huku huwaweki wazi watu wengine hakuna atakayekuona mtaalamu hata kidogo.
4.UADILIFU:
Utaonekana mtaalamu ikiwa utakuwa unasimamia kanuni za shughuli yako.Hakuna anayependa kumpa kazi mtu asiyejua kufuata kanuni za kazi yake.
5.HESHIMA:
Kama huna heshima kwa watu wengine unaofanya nao au unaowafanyia shughuli basi hautaonekana mtaalamu hata kidogo.
6.ONGEZA UJUZI:
Tafuta ujuzi wa ziada,usiendelee kung’ang’ania ujuzi ule ule kila siku. Toka nje ya yale unayoyafahamu ili kupata mengine mapya kuongezea katika yale unayayafahamu ili kuboresha zaidi utendaji.
7.MTAZAMO CHANYA:
Kama wewe kila siku unaangalia makosa tu bila kuwa na mtazamo chanya juu ya shughuli unayofanya kuwa mtaalamu itakuwa ndoto kwako.
8.TOA MSAADA:
Wasaidie wenzako unaofanya nao shughuli sio kwa kuwa wewe unafahamu kitu fulani basi hutaki wenzako wafahamu.
Waonyeshe jinsi ya kufanya kazi vizuri pale unapoweza na wasikilize pale wanapokuuliza maswali.
9.TENGANISHA MATUKIO:
Usihusishe matukio ya nyumbani au mtaani na kazi,ukiwa katika shughuli zako weka mawazo yako yote hapo.Utakuwa mtu wa ajabu kufika eneo la kazi na kuanza kushughulikia masuala ya nyumbani huku ukiacha kazi haziendi.
10.KUWA MSIKIVU:
Kila mtu ana hitaji la kusikilizwa pale anapokuwa na jambo la kusema,Kwa hiyo wape watu nafasi ya kukuelezea yale wanayodhani yatasaidia katika utendaji wa kazi.
KILA MMOJA WETU ANAPENDA KUPATA MAFANIKIO KATIKA SHUGUHULI ILE ANAYOFANYA,BASI TUANZE SASA KUFANYA KAZI KITAALAMU ILI TUWEZE KUFIKIA YALE TUNAYOYATAKA.