Home Elimu Wahitimu BoT watakiwa kutumia ujuzi kuimarisha sekta ya fedha

Wahitimu BoT watakiwa kutumia ujuzi kuimarisha sekta ya fedha

0 comment 18 views

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, amewataka wahitimu wapya wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania kutumia maarifa na ujuzi waliopata kwa uadilifu na weledi ili kusaidia kuimarisha sekta ya fedha nchini.

Akizungumza katika Mahafali ya Tatu ya Chuo hicho yaliyofanyika Oktoba 31, 2024 jijini Mwanza, Gavana Tutuba amesisitiza kuwa sekta ya fedha ni mhimili wa uchumi wa taifa, hivyo inahitaji wataalamu waaminifu wenye maadili na ujuzi wa hali ya juu.

Baadhi ya wahitimu wapya wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania.

“Nawasihi kutumia elimu na ujuzi mlioupata kulitumikia taifa letu kwa weledi, uadilifu na uzalendo mkubwa. Muwe kioo na tunda la Benki Kuu ya Tanzania, na kuwa mfano bora kwenye sekta ya fedha,” amesema Gavana Tutuba.

Ameongeza kuwa Benki Kuu inafuatilia kwa karibu wafanyakazi wote wa sekta ya fedha na haitasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya wizi au udanganyifu.

Akizungumza kuhusu changamoto za ajira kwa vijana, Gavana Tutuba amehimiza wahitimu kuwa wabunifu, wachapakazi, na kutumia ipasavyo ujuzi waliopata. Amesema mfumo wa kujifunza wa vitendo unaotumika chuoni hapo unawapa wahitimu uwezo wa kukabiliana na ushindani wa ajira na pia kuwajengea uwezo wa kujiajiri.

“Ujuzi huu utawasaidia sana katika kuingia kwenye soko la ajira na kujiajiri,” ameongeza Gavana.

Aidha, amewasisitizia umuhimu wa kujiendeleza kitaaluma na kitaalam kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na uchumi duniani.

“Kuhitimu kwenu siku ya leo kuwe ni chachu na mwanzo wa safari mpya ya kujifunza na kupata maarifa mapya katika maeneo na viwango mbalimbali,” amewaasa wahitimu hao.

Akizungumza awali, Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Dkt. Nicas Yabu ameeleza kuwa katika kuboresha sekta ya fedha nchini, zaidi ya watoa huduma ndogo za fedha 1,280 wamepata mafunzo kupitia programu maalum ya muda mfupi (Crush Programme), huku wahitimu 103 wakitunukiwa vyeti vya umahiri kwenye sekta hiyo.

Katika mahafali hayo, wahitimu 40 wamekutunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki na wahitimu 38 wametunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter