Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam kuhusiana na majukumu yake katika kusimamia Uchumi wa nchi.
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika Machi 2025 washiriki walipata fursa ya kujifunza namna Benki Kuu inavyoandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.
Aidha, wameelimishwa kuhusu jukumu la Benki la Kuu la kuchapisha sarafu ya nchi ambayo ni shilingi ya Tanzania pamoja na namna yakutambua alama za usalama katika noti na utunzaji sahihi wa noti hizo.
Vilevile, wameelezwa juu ya zoezi la kuondoa katika mzunguko noti za zamani za shilingi 20, 200, 500, 1000, 2000, 5000 na 10000. Noti hizo zinazoondolewa ni za matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003, na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010. Zoezi hilo lilianza tarehe 6 Januari 2025 na linaendelea mpaka tarehe 5 Aprili 2025.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa jitihada za Benki Kuu za kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kwenye jamii kwa lengo la kukuza uelewa wao kuhusu masuala ya fedha ili kuwawezesha kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi.