Home FEDHA Benki Kuu yashiriki mkutano wa taasisi za fedha Afrika (AFIS) 2024

Benki Kuu yashiriki mkutano wa taasisi za fedha Afrika (AFIS) 2024

0 comment 46 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashiriki katika Kilele cha Mkutano wa Taasisi za Fedha Afrika 2024, maarufu kama AFIS, unaofanyika jijini Casablanca, Morocco, kuanzia tarehe 9 hadi 10 Desemba 2024.

Mkutano huu ni jukwaa muhimu linalowakutanisha watunga sera za fedha na uchumi, taasisi za kifedha, na wawekezaji wa mataifa ya Afrika kujadili na kuendeleza mageuzi ya kiuchumi katika bara hili.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera na Uchumi), Dkt. Yamungu Kayandabila, alielezea mafanikio ya Tanzania katika kuendeleza ushirikiano kati ya waendeshaji wa huduma za kifedha katika makampuni sita ya simu yaliyopo nchini Tanzania, hali iliyowezesha huduma za fedha kwa njia ya mitandao ya simu kufanyika kwa urahisi.

“Kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo ya papo kwa hapo Tanzania (TIPS) na Benki Kuu kumechangia kupunguza gharama za miamala kwa watumiaji wa huduma hizo. Aidha, Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuwezesha biashara za kikanda,” alisema Naibu Gavana.

Aidha, alisema kuwa kuongezeka kwa wanachama wapya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kunaibua changamoto na fursa, akiwahamasisha wawekezaji kutafuta suluhisho za kibunifu katika fursa hii inayojitokeza hivi sasa.

Katika majadiliano hayo, yaliyokuwa na mada: “Kukuza Muingiliano wa Mifumo ya Mitandao ya Kifedha Barani Afrikaa,” masuala muhimu na fursa za kuimarisha ujumuishaji wa huduma za kifedha na mifumo ya malipo baina ya nchi za Afrika yalijadiliwa.

Ushiriki wa BoT katika kilele cha Mkutano huo unaonyesha dhamira yake ya kushirikiana kikanda, kuleta ubunifu katika mifumo ya kifedha, na kukuza maendeleo ya kiuchumi endelevu.

Mapema, wakati wa hafla ya ufunguzi Mustapha Rawji, Mtendaji Mkuu wa RawBank kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alizungumza kuhusu mada ya “Mikopo ya Kibiashara: Kupunguza Tofauti na Benki Shirikishi” (Trade Finance: Bridging Africa’s Correspondent Banking Gap) ambapo aliwahimiza wataalamu wa masuala ya fedha wa Afrika kubadilisha mtazamo kuhusu mahitaji ya kifedha na kuyaona kama fursa badala ya changamoto.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter