Mapendekezo yamepitishwa kwa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC) leo 23 Juni, 2022 wamepitisha mapendekezo ya hayo.
Wajumbe hao wamepitisha mapendekezo hayo kwenye semina iliyoandaliwa na Wizara ya Afya ya kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini iliyofanyika kwenye ukumbi wa White house jijini Dodoma.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hatua hiyo inapelekea Wizara ya Afya kwenda kutunga sheria ya Bima ya Afya kwa wote na kuongeza kuwa kiasi kitakacholipwa na mwananchi kwa mwaka kitamwezesha kupata huduma za matibabu kama mtumishi wa Serikali, kuanzia ngazi ya Zahanati, Kituo cha Afya, hospitali ya Wilaya, Rufaa za Mkoa, Kanda, Maalumu na hata Taifa ya Muhimbili.
“Hii itasaidia kwa Watanzania wote kupata huduma bora za Afya bila kikwazo cha fedha pia Serikali itahakikisha Dawa zinapatikana kwa wakati na zinazokidhi mahitaji ya wagonjwa,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa na bima ya afya kwa wote ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Ibara ya 83(e) cha kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwemo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote.