Kampuni ya Bima ya Strategis imetangaza kuanza utoaji wa bima ya mazao kwa wakulima ili kuwaongezea tija pamoja na uhakika wa uzalishaji. Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Kain Mbaya ametangaza nia hiyo wakati kamouni ikizindua mpango mpya wa huduma za bima ambapo ameeleza kuwa, mifumo ya utoaji bima ya jumla imekamilika na bima za kilimo zitapatikana ndani ya miezi miwili ijayo.
Mbaya amefafanua kuwa, wakulima hasa wale wa vijijini ndio walengwa wakubwa wa mpango huo wa bima na kampuni hiyo imejipanga kuwafikia hata kwa kutumia mifumo ya kidigitali.
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima nchini Dk. Baghayo Saqware amesema sekta imara ya bima ina mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa viwanda hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Bima nchini (TIRA) itaunga mkono jitihada zinazofanyika kukuza upatikanaji wa huduma hiyo. Kwa upande wa bima kwa wakulima, Dk. Saqware amesema hitaji hilo limekuwepo kwa muda mrefu na TIRA ilishaanza kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuanzisha bima yao kwa kuzingatia mahitaji lakini hawakufanikiwa.