Mkurugenzi wa Leseni na Mwenendo wa Soko kutoka Mamlaka ya Bima Tanzania, Samweli Mwiru ametoa wito kwa wakulima hapa nchini kujiandaa na ujio wa bima katika mashamba yao huku akiwataka kutambua umuhimu wa kuwa na bima katika kilimo.
“Bima itasaidia endapo patatokea majanga yoyote katika kilimo na mazao, makampuni ya bima nchini yataweza kuwalipa hizo gharama ili kumfanya mkulima kutofilisika na kumfanya aendelee na shughuli zake za kilimo”. Ameeleza Mwiru.
Mbali na hayo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa bima ya kilimo itamlinda mkulima katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na majanga yanayosababishwa na hali ya hewa, majanga yanayotokana na magonjwa mbalimbali ya mimea na kusisitiza kuwa bima hiyo italenga zaidi kukinga majanga yatokanayo na hali ya hewa.
Takribani asilimia 70 ya watanzania wote ni wakulima hivyo kuanzishwa kwa bima kwenye kilimo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuepuka majanga ambayo wakulima hukumbana nayo mara kwa mara kama vile moto, mafuriko na magonjwa ya mazao.