Home BIASHARA Fukwe sasa kuchochea utalii

Fukwe sasa kuchochea utalii

0 comment 37 views

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali imejipanga kuimarisha matumizi ya fukwe na kuzifanya kuwa sehemu ya kivutio cha utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaofika hapa nchini, kutengeneza ajira kwa wananchi na vilevile kukuza uchumi wa taifa. Majaliwa amesema hayo kwenye ufunguzi wa onyesho la kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo ambapo alimuwakilisha Rais John Magufuli.

Onyesho hilo la siku tatu linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam linahudhuriwa na wafanyabiashara wakubwa wa utalii wapatao 170  kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na wauzaji wa bidhaa za utalii wanaofikia 300 kutoka ndani na nje ya nchi.

Waziri Majaliwa ameeleza kuwa, sekta ya utalii inachangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo yote ya nje na imeajiri watu wapatao 1,500,000. Majaliwa amedai kuwa kutokana na juhudi za utangazaji wa vivutio vya utalii nchini unaoratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wageni wameongezeka na wamekuwa wakifika kuona vivutio huku wakitambua kuwa Tanzania ni nchi ya amani, yenye utulivu na watanzania ni watu wakarimu.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu amemshukuru Rais Magufuli kwa jitihada zake kwenye maendeleo ya sekta ya utalii nchini kutokana na hatua ambazo amekuwa akichukua ili kukuza sekta hiyo.

“Ununuzi wa ndege saba mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambapo ndege nne tayari zimeshawasili na kuanza kutoa huduma ni kielelezo tosha cha juhudi za serikali. Kati ya ndege hizi zipo ambazo hivi karibuni zitaanza kutoa huduma ya usafiri kati ya Tanzania na nchi za India na China”. Ameeleza Majaliwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter