Home FEDHA Elimu ya fedha muhimu kwa vijana

Elimu ya fedha muhimu kwa vijana

0 comment 146 views

Kwa bahati mbaya, elimu kuhusu fedha binafsi haitolewi mashuleni au vyuoni. Hivyo watu hasa vijana wanaweza kutokuwa na uelewa kuhusu matumizi ya fedha pale wanapoanza kujitegemea na kuishi maisha bila ya msaada wa wazazi au walezi. Kila kitu kina muda wake, hivyo ili kuishi maisha mazuri yenye mafanikio vijana wanatakiwa kuzingatia yafuatayo kuhusu fedha;

Jifunze kujinyima. Sio kila mtu hujifunza tangu utotoni kuhusu kujinyima, hivyo kama una uelewa na uwezo wa kujinyima ni jambo zuri. Sawa unaweza kuhitaji au kutamani kitu lakini unatakiwa kujiuliza, je ni lazima ukinunue kitu hicho kwa muda huo au unahitaji kuwekeza fedha kwa muda fulani ili uweze kulipia kitu hicho? Kama unaweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu vitu unavyotaka itakuwa rahisi kumudu fedha zako na matumizi.

Thibiti maswala ya kifedha kwa ajili ya siku zijazo. Ikiwa unashindwa kusimamia fedha zako watu wengine watafanya hivyo. Wengine watakuwa na nia nzuri na wengine watakuwa na nia mbaya. Hivyo jitahidi kujua kuhusu fedha kwanza na namna ya kuthibiti matumizi yake ili kuhakikisha siku zijazo hutopata shida. Sio lazima kuomba ushauri kila wakati, unaweza kujifunza kuhusu fedha kwa kusoma vitabu, makala, kusikiliza redio zinazohusu mambo ya fedha.

Jua fedha zako zinaenda wapi. Jitahidi kuandika matumizi yako ili kujua fedha zako zinatumika katika mahitaji gani. Sio vyema kutumia fedha zaidi ya kipato chako hii itakuletea shida. Jitahidi kuweka bajeti, ili uweze kunufaika zaidi baadae.

Hata kama unalipwa fedha kidogo kiasi gani, hakikisha unajilipa hii itakusaidia kuweka fedha kwa ajili ya mambo ya ghafla au ya mbeleni. Unaweza kuweka fedha kwenye akaunti za akiba, au unaweza kuwekeza katika masoko ya hisa ili iwe inaongezeka.

Anza kuweka akiba mapema, kujiandaa na kustaafu mapema kutapunguza kazi ya kuwekeza hapo baadae. Na kazi kwako itakuwa ni chaguo na si lazima ufanye kazi ili kuingiza kipato kwa sababu utakuwa na uwezo wa kuwekeza katika mambo mengine mbalimbali hivyo kazi itakuwa ni namna moja wapo ya kujipatia kipato.

Wakati unakubali kufanya kazi katika kampuni fulani unatakiwa kufikiria kama mshahara wanaotaka kukupa utakutosha kwa kiasi gani katika matumizi yako hata baada ya kukatwa kodi. Hivyo hakikisha una uelewa wa masuala ya kodi hasa kodi zinazokatwa katika mshahara wako ili kujua unajipangaje ili kukamilisha malengo yako ya muda mfupi na muda mrefu.

Watu wengi hawaoni umuhimu wa bima, lakini kuwa na bima katika masuala mbalimbali ni muhimu ili kama jambo lolote litatokea basi iwe rahisi kupata huduma kuliko kutumia fedha nyingi kwa wakati mmoja. Hivyo angalia mambo ambayo unatumia fedha nyingi au unaweza kutumia fedha nyingi ikiwa changamoto itatokea na kuweka bajeti kwa ajili ya bima ya mambo hayo.

Jambo unalotakiwa kukumbuka zaidi ni kuwa huhitaji kuwa na elimu kubwa sana kumudu matumizi ya fedha zako. Jenga mfumo mathubuti kulingana na kipato chako ili kurahisisha matumizi yako ya fedha na kutimiza malengo yako ya sasa na ya baadae.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter