Kikawaida watu wanafanya kazi au kujishughulisha kwa bidii ili siku moja wawe Matajiri, na waweze kuishi kwa raha na furaha. Ili kufanikisha hilo ni muhimu kuwa na mfumo katika maisha yako hasa kwenye kipato unachokipata na matumizi yako.
Hatua ntakazozitaja ni rahisi kwa kuzisoma lakini si rahisi kuzitekeleza, hivyo ni muhimu kuwa na malengo ambayo yatakukumbuasha umuhimu wa kufuata hatua hizo ili baadae ufurahie kazi ya mikono yako/matunda ya shughuli unayofanya kwa bidii.
Hizi ni hatua tatu zitakazokusaidia kujipatia utajiri:
- kutengeneza fedha
- kuweka akiba
- kuwekeza
KUTENGENEZA FEDHA
Hapa swala sio kutengeneza fedha pekeake, unashauriwa kujiuliza je unatengeneza kipato cha kutosha? Ukishapata jibu hapa inakuwa rahisi kuamua kama kuna umuhimu wa kupunguza matumizi hasa yale yasiyo muhimu ili kuhakikisha fedha unayotumia haitumiki bila mpangilio. Kama una kipato kidogo unashauliwa kuangalia njia mbadala zitakazokusaidia uongeze kipato chako. Kwamfano baada ya kutoka katika kazi yako ya kila siku unaweza kufanya kitu unachopenda na kupata fedha kupitia kitu hicho mfano:uchoraji, uimbaji kwenye bendi, kupiga picha, kupika keki nk.
La muhimu ni kutumia fursa zilizopo au unazoziona ili kuongeza kipato chako.
KUWEKA AKIBA
Unatengeneza fedha za kutosha, unaishi vizuri, huna sababu yakutojiwekea akiba hasa kama una malengo ya kuwa tajiri hapo baadae. Hivyo ni muhimu kutengeneza bajeti ili kuweza kuweka akiba. Kwanza jaribu kuandika matumizi yako yote ya mwezi mzima ili kujua fedha zako zinaenda wapi na mambo gani yanahitaji fedha kwa mfano chakula,malazi,mavazi na vitu gani unatakiwa kuacha kufanya kwasababu si vya muhimu na vinatumia fedha.
Hii haimaanishi kwamba ujinyime kabisa, hapana kwamfano kama umezoea kununua nguo kila wiki unaweza kupunguza na kununua mara moja kwa mwezi. Au kama umezoea kula chakula kwenye migahawa ya bei kila siku mchana unaweza kupunguza na kwenda mara mbili kwa mwezi au mara moja kwa wiki. Ili mradi mwisho wa siku akiba yako iwe inaeleweka.
KUWEKEZA
Baada ya kujiwekea akiba kwa kipindi fulani (utaamua muda), fikiria namna ya kuwekeza fedha hizo. Ili ziweze kuzaliana zaidi. Mara nyingi huwa wanashauri kuongea na mtaalamu wa maswala ya ushauri ili kuweza kuamua mawazo mazuri. Kwasababu wao huwa wanajua zaidi kuhusu uwekezaji, labda kama una ujuzi basi unaweza kuamua wapi uwekeze. Usiwe muoga wa kuwekeza, kwani uwekezaji ndio chanzo cha safari ya kuelekea kwenye utajiri.