Ili kulinda mazingira kuna umuhimu sana wa kuchakata vile vitu ambavyo vinaweza kuwa si rafiki katika mazingira. Hivyo unaweza kujipatia fedha kwa kufanya mchakato huo na kulinda mazingira kwa mara mmoja. Hivyo basi hivi ni baadhi ya vitu ambavyo unaweza kuchakata na kujipatia fedha kwa uharaka zaidi:
Chupa
Kuna chupa za kila aina kwa mfano chupa za plastiki, chupa za glasi na chupa za bati ambazo hutumika kuhifadhi maji, mafuta, mvinyo nk. Hivyo kwa kuzikusanya chupa hizo unaweza kuwauzia wazalishaji wa bidhaa hiyo na kujipatia fedha. Kwamfano mtaani kuna watu wanajipatia kipato chao cha kila siku kwa kupitia kazi ya kuokota chupa za maji na kwenda kuuza. Vilevile watu hasa wanawake wanaweza kujipatia fedha kupitia chupa za kuhifadhia vipodozi kwa kuwauzia wazalishaji wa vipodozi hivyo ambao mara nyingi hufurahishwa na wateja ambao hurudisha chupa na makopo baada ya matumizi ya bidhaa zao.
Samani
Badala ya kutupa samani za zamani zilizopo nyumbani kwanza unaweza kujipatia fedha kupitia samani hizo kwa kuzirekebisha na kuuza. Na ikiwa huna uwezo wa kurekebisha unaweza kuwauzia watu ambao hununua bidhaa ambazo zimetumika, ambao mara nyingi hununua bidhaa zilizotumika na kuziboresha na kuziuza kwa bei kubwa zaidi ili kupata faida. Kwa urahisi zaidi unaweza kuwapata watu hao katika mitandao ya kijamii.
Vyuma chakavu
Inaelezwa kuwa vyuma, ni moja ya malighafi ambayo huchakatwa zaidi duniani kwa sababu ya uwezo wake wa kuchakatwa mara nyingi bila kupunguza ubora wake. Hivyo kuna maeneo mengi tu ambayo huwa yako tayari kununua vyuma chakavu kulingana na ukubwa na uzito wa vyuma hivo. Hivyo badala ya kutupa vyuma ambavyo vimechakaa kwa mfano vyuma vya kwenye gari, unaweza kuuza na kujipatia fedha za ziada.
Matairi ya gari
Ikiwa matairi ya kwenye gari yako yamechakaa unaweza kujipatia fedha za haraka kupitia matairi hayo kwa kuwauzia watu wanaopanda maua ambao hutumia matairi pia ili kupendezesha muonekano, pia unaweza kuuza kwa watu ambao huyarekebisha kisha kuuza kwa faida. Unaweza kuwapata watu hao katika gereji za magari na sehemu za kujazia upepo wa vyombo vinavyotembea. Kadri siku zinavyokwenda watu wanaendelea kuwa wabunifu hivyo unaweza kuwauzia matairi watu ambao wanatengeneza viti vya kukalia na meza.
Vifaa vya kielektroniki
Kama una simu ambayo ni mbovu au imeharibika unaweza kuuza na kujipatia fedha. Kwani watu ambao hutengeneza simu hupendelea kununua vifaa hivyo kwa ajili ya kurekebishia vifaa vingine vya kielektroniki, mbali na mafundi wa simu siku hizi unaweza kuuza simu ya zamani au kununua simu ilivyotumika katika tovuti kama Gazelle na kujipatia fedha.