Halmashauri ya Mji wa Mbinga imepokea jumla ya Shilingi bilioni 11.974 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Amina Seif amesema hivi karibuni kiasi hicho kilitumika kutekeleza miradi mbalimbali kwenye sekta za Elimu, Afya, Maendeleo ya jamii, Kilimo, Utawala, Biashara na Mifugo.
Ameeleza kuwa fedha hizo zimetolewa katika kipindi cha karibia miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amina ameyasema hayo katika Manispaa ya Songea wakati wa mkutano uliowaleta pamoja wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa kutoka Mkoa wa Ruvuma kuelezea mafanikio ya uongozi wa awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Amina.
Amebainisha kuwa Halmashauri katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipokea jumla ya shilingi bilioni 5.6, mwaka 2022/2023 bilioni 5.4 na mwaka 2023/2024 hadi kufikia mwezi Desemba 2023 Halmashauri ilipokea shilingi Milioni 974.6.
Katika sekta ya elimu, amesema kwa kipindi cha miaka mitatu Halmashauri imepokea shilingi bilioni 7.8 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika sekta ya elimu ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 182 , ujenzi wa shule mpya 4 ambazo ni sekondari ya Lusonga, shule ya msingi Kipika , shule ya msingi Mpepai na shule ya sekondari Matarawe.
Miradi mingine ni nyumba za walimu 4 katika shule ya sekondari Lusonga na shule za msingi Pachasita, Miembeni , Ruvuma chini na Kihungu, Ujenzi wa matundu ya vyoo 186 katika shule mbalimbali za msingi na sekondari na Ujenzi wa vyumba vya maabara 10 katika shule za sekondari Luhuwiko ,Kilimani, Lamata na Kagugu.
Katika sekta ya Afya kwa kipindi hicho, Halmashauri imepokea shilingi bilioni mbili kwaajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo viwili vya afya vya Mbangamao na Myangayanga , ujenzi wa zahanati 9 katika vijiji vya Makatani, Matarawe, Kihuka, Lupilo, Njomlole, Mahande na Kitelea.
Katika sekta ya Maendeleo ya Jamii, kwa kipindi cha miaka mitatu Halmashauri imepokea na kutumia shilingi bilioni 2.64 kwaajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhawilishaji fedha katika kaya maskini na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Wakati kiasi cha shilingi bilioni 2.03 kikitumika katika uhawilishaji wa fedha katika kaya maskini, shilingi milioni 609.9 imetolewa kwa vikundi 70 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Pia Mkurugenzi amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Halmashauri ilikusanya na kutumia kiasi cha shilingi milioni 570 kutekeleza miradi katika idara za kilimo, mifugo, biashara, fedha, Ardhi, mipango na utawala.
Miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa ofisi za Kata na vijiji, ununuzi wa Pikipiki 27 ,upimaji wa viwanja 2200 na usimamizi na huduma za ushauri kwa wakulima ili kuongeza tija kwa wakulima.