Na Mwandishi wetu
Mbunge wa Mbarali mkoanu Mbeya ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu hapa nchini Haroon Pirmohamed ametumia zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi minne ya maendeleo katika jimbo lake.
Mbunge huyo mwenye kaulimbiu inayosema “Maneno kidogo, kazi zaidi” amesema atawasaidia wananchi wake pale watakapokwama na hatojali kutumia rasilimali zake pamoja na fedha za mfuko wa jimbo kuhakikisha shughuli za kimaendeleo hazikwami jimboni kwake.
Katika awamu ya kwanza jumla ya trekta ndogo maarufu kama powertiller 115 zilitolewa ambapo kila kijiji wilayani hapo kilifanikiwa kupata trekta moja na kuendesha shughuli zao za kilimo. Miradi mingine iliyowezeshwa na mbunge huo ni pamoja na uchimbaji wa visima 10 uliogharimu Sh 129 milioni na ugawaji wa bati 4000 kwa kata saba. Kila kata ilipatiwa mabati 200 ili kujenga vyoo kwenye shule za msingi na sekondari.
Hivi sasa mbunge huyo anatoa mifuko ya saruji kwenye kila kijiji na mtaa ambapo ametumia takribani Sh 105 milioni, lengo likiwa ni kuwezesha ujenzi wa mashule, zahanati na miradi mingine ambayo vijiji hivyo vinahitaji.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune amempongeza mbunge huyo kwa juhudi anazozifanya ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.