Mikopo inayotolewa na benki huwa na faida nyingi, lakini ni hatari pia kwako na mkopeshaji. Mkopeshaji huingia katika hatari ya kukukopesha fedha ili hali akijua kuwa unaweza kutolipa fedha zote. Na katika upande wako wa fedha unaweza kupoteza fedha au kupoteza mali kama nyumba. Ndio maana wakopeshaji hujitahidi kuweka viwango ambavyo ni rafiki katika pande zote mbili.
Hivyo ikiwa umefanya maamuzi ya kukopa unatakiwa kujua haya:
Mkopo siku zote huongeza gharama za ziada. Hata kama una bajeti yako lakini kuwa na mkopo huathiri mapato yako kwa namna moja au nyingine kwasababu kila mwezi au baada ya muda fulani unatakiwa kufanya malipo ya mkopo huo. Hivyo ikiwa unataka kukopa unatakiwa kujua kuwa mabadiliko yatafanyika katika mfumo wako wa kifedha. hivyo hakikisha una mpango mathubuti wa kulipa mkopo wako ili kuepusha changamoto zozote za kifedha zinazoweza kutokea kutokana na mkopo unaotaka kuchukua.
Kutolipa mkopo kwa wakati kunaweza kuharibu historia yako ya ukopaji. Kuwa na historia nzuri ya kukopa na kurejesha husaidia pale ukiwa unahitaji mkopo mwingine au mkubwa zaidi. Hivyo hakikisha unalipa mkopo wako ndani ya muda ili kuepukana na historia mbaya ya ukopaji kwasababu si rahisi kurejesha historia nzuri na lazima itachukua muda mrefu kurudisha uaminifu kwa taasisi za kifedha hususani benki kukuamini na kukukopesha tena.
Ikiwa utawekeza mali ili kupata mkopo unatakiwa kujua kuwa benki hufuata sheria na makubaliano ya mkopo husika hivyo kama uliwekeza kiwanja na ukashindwa kulipa mkopo basi benki itachukua mali hiyo ili kuweza kujilipa na kuepuka na hasara. Ndio maana ni muhimu kutathmini athari itakayotokea ikiwa umeweka mali zinazotumika kwamfano nyumba ya familia kabla ya kuwekeza mali husika. Kwa wafanyabiashara inashauriwa kuepuka kuchanganya mali binafsi na za biashara ikiwa unataka kuomba mkopo kupitia mali.
Vilevile benki pia huwa zinakuwa katika hatari kwa kutoa mikopo hasa kwa watu ambao hawarudishi mikopo hiyo. Ikiwa benki ina historia kubwa ya kutorejeshewa mikopo hupata athari sana na kuathiri masoko, pamoja na kuongeza viwango ili kuweza kufidia. Kwa kufanya hivyo uchumi kwa ujumla lazima upate athari.
Hivyo inashauriwa kwa wakopeshaji kuwa na mpango wakiwa wanataka kukopa katika taasisi yoyote ya kifedha kwamfano kwanza ni muhimu kuwa na sehemu ya kujipatia kipato, na mkopo huo ni vyema zaidi kama utaelekezwa katika biashara au namna ambayo itatengeneza fedha zaidi ili kurahisisha swala zima la ulipaji.