Home FEDHAMIKOPO Ombi lako limekataliwa? Fanya hivi

Ombi lako limekataliwa? Fanya hivi

0 comment 110 views

Mara nyingi mtu akituma maombi hutegemea kukubaliwa maombi yake. Kutokubaliwa ombi siku zote si habari njema kwa mtu aliyetuma maombi. Sio vibaya kukopa lakini kuwa na historia mbaya ya ukopaji ni moja ya mambo ambayo yanaweza kukusababishia ukose mkopo. Hivyo ikiwa umeomba mkopo na kukataliwa jitahidi kuangalia sababu ambazo zinaweza kuwa zimesababisha ukose mkopo huo.

Kwa bahati nzuri wakopeshaji wengi hujitahidi kuwa wakweli kwa kuelezea sababu ya mkopaji kukosa mkopo husika. Baadhi ya mambo ambayo yanaweza kukusababisha ukose mkopo ni haya:

Historia ya ukopaji, kutokopa kabisa kunaweza kusababisha ukose mkopo, na ikiwa una historia ya kukopa mkopeshaji ataangalia historia yako ya kukopa na kurudisha mikopo ili afanye maamuzi. Ikiwa hii ndio sababu iliyosababisha ukose mkopo basi mkopeshaji atakuelezea.

Kipato chako kinaweza kusababisha ukose au upate mkopo. Mkopeshaji ataangalia kiasi cha fedha unachoingiza na kutathmini kama unaweza kulipa mkopo ulioomba. Na ndio maana hata katika mikopo binafsi, baina ya marafiki au ndugu inashauriwa kujua uwezo wa kifedha alionao mkopaji ili kuepusha malumbano ikiwa mkopaji akashindwa kulipa.

Nini cha kufanya:

Kukosa mkopo mara moja haimaanishi kuwa utakosa siku zijazo. Ndio maana kuna umuhimu wa kuuliza maswali katika kila jambo linalotokea. Hivyo baada ya kukosa mkopo katika sehemu husika uliza maswali  ya kutosha katika taasisi husika ya kifedha au mtu binafsi vigezo walivyotumia kutathmini kama unafaa au hufai kupata mkopo husika.

Baada ya kujua sababu zilizosababisha ukose mkopo, fanya marekebisho. Kama una madeni jitahidi kulipa, kama ni sababu nyingine binafsi zirekebishe ili uweze kuomba tena mkopo. Taasisi za fedha huangalia pia historia yako ya kulipa mikopo kila mwezi hivyo kama kuna tatizo katika hilo fanya marekebisho.

Pia ikiwa umekataliwa mkopo unaweza kutumia vitu vyenye thamani kupata mkopo huo. Lakini kuwa makini na vitu utakavyoweka ili kupata mkopo huo kwani watu wengi wamepata changamoto kama kunyang’anywa nyumba,gari n.k kwa sababu ya mikopo. Hivyo tafakari kwa makini kabla hujawekeza mali kwa ajili ya mkopo na angalia athari zinazoweza kutokea ikiwa umeshindwa kulipa mkopo huo. Ni muhimu kuhakikisha maamuzi yako hayaathiri watu wengine.

Taasisi za fedha hutoa mikopo watu wenye wadhamini, hivyo ikiwa umekosa mkopo unaweza kutafuta mdhamini ili kuweza kupata mkopo husika. Hakikisha mdhamini huyo ana vigezo ikiwa ni pamoja na historia nzuri ya ukopaji, uwezo wa kifedha n.k kwani mkopeshaji ataangalia vigezo kama hivyo ili kuidhinisha mpango mzima wa mkopo.

Kukosa mkopo sehemu moja haimaanishi kuwa utakosa sehemu nyingine. Hivyo ikiwa umekosa mkopo katika taasisi moja jaribu katika taasisi nyingine. Hivyo kama umekosa katika taasisi kubwa kama benki jaribu katika taasisi ndogo ambazo zimejikita zaidi katika kuinua maisha ya watu wa hali ya chini.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter