Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa jitihada zake za kusaidia wakulima wadogo na kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kuinua kipato chao. Samia amesema hayo wakati akikabidhi hundi ya mfano ya Sh. 1.285 bilioni zilizotolewa na benki hiyo kwa ajili ya miradi ya kilimo cha alizeti kwa wakulima wapatao 458 walio chini ya vyama vya ushirika (AMCOS) mkoani Singida.
Makamu huyo amewataka wakulima walionufaika na mkopo huo kutumia fedha hizo kuongeza tija ya uzalishaji ili kufanikisha malengo ya mkopo huo, ambayo ni kusaidia sekta ya mbegu za mafuta nchini ili kutatua changamoto za ukosefu wa mafuta. Mbali na hayo, pia amewataka viongozi wa ushirika kuhakikisha mkopo huo unatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha unarudi kwa wakati uliopangwa.
“Nawasihi muwe waaminifu kwa kuutumia mkopo huu vizuri na kuurudisha kwa wakati ili kuwawezesha wakulima wengine nchini waweze kukopeshwa ili kuchagiza uzalishaji wa mazao ya kilimo”. Amesema Makamu wa Rais.
Naye Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Augustino Matutu Chacha, amesema kwa mwaka 2018/2019, benki hiyo imepanga kutoa mikopo ya jumla ya Sh. 3.506 bilioni kwa miradi ya kilimo mkoani Singida pekee.