Home FEDHAMIKOPO Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia wasaini mikataba ya shilingi bilioni 248

Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia wasaini mikataba ya shilingi bilioni 248

0 comments 207 views

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) wamesaini mikataba miwili yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104, sawa na takriban shilingi bilioni 248, kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia nchini Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba  kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Nathan Belete.

Akifafanua kuhusu mikataba hiyo, Dkt. Nchemba amesema kuwa mkataba wa dola za Marekani milioni 4, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 9.5 ni msaada na Mkataba wa dola za Marekani milioni 100, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 238 ni mkopo wenye masharti nafuu.

Amesema mradi wa PAMOJA uliosainiwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanawake pamoja na huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia Tanzania Bara na Zanzibar.

‘’Hili litatimizwa kupitia uimarishaji vikundi vya wanawake kwa kuwajengea ujuzi wa biashara na kuwaunganisha na fursa za masoko, kuongeza fursa za mikopo nafuu kwa vikundi vya wanawake, kuwaongezea upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo rasmi ya kifedha pamoja na kuimarisha huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia”, alifafanua Mhe. Dkt. Nchemba,

Amesema mradi huo utawanufaisha moja kwa moja wanawake wapatao 319,850 na walengwa wengine 399,000, wakiwemo wanafamilia za wanufaika.

Amesistiza kuwa kukuza usawa wa kijinsia si suala la wanawake pekee bali ni msingi wa Taifa la kidemokrasia, lenye haki na linalostawi na kuongeza kuwa kuondoa tofauti za kijinsia kunaboresha uzalishaji na kuimarisha uhimilivu wa kiuchumi.

“Mradi wa PAMOJA ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa 2021/22 – 2025/26, Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 na pia ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amelipa kipaumbele suala la usawa wa kijinsia”, amesema Dkt. Nchemba.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!