Uhitaji wa mikopo ya fedha kwa ajili ya kuendesha biashara na shughuli mbalimbali umetajwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa nchini.
Rodrick Kailembo ni Meneja Masoko wa K-Finance wanaotoa huduma ya mikopo ya fedha anasema “kwa sasa kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa mikopo, wateja wanaongezeka sana. Biashara nyingi ziliyumba wakati wa ugonjwa wa Corona na sasa wafanya biashara wanajaribu kuimarisha biashara zao”.
K-Finance ambao wanatoa mikopo kwa wafanyabiashara na waajiriwa wanasema licha ya uhitaji kuwa mkubwa, wajasiriamali wengi wadogo wanashindwa kupata mikopo kutokana na kutokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ikiwemo biashara zao kutorasimishwa.
“Tunatoa mikopo kuanzia shilingi milioni moja hadi milioni 50 kwa wafanyabiashara ambao biashara zao zimerasimishwa. Pia tunatoa kwa waajiriwa,” ameeleza Kailembo.
Amefafanua kuwa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ambao biashara zao zimerasimishwa, wanatakiwa kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN Number) na kadi ya gari kama dhamana ya mkopo.
Kwa upande wa waajiriwa, Kailembo amesema mwombaji anatakiwa awe na mkataba wa kazi pamoja na kadi ya gari ama hati ya kiwanja kama dhamana ya mkopo ambapo mikopo hiyo ni kuanzia muda wa mwezi mmoja hadi kumi na mbili.
Akizungumzia wajasiriamali wadogo ambao wengi biashara zao hazijarasimishwa huku wengi wao wakikosa dhamana ya kupata mkopo amesema hiyo ni changamoto kubwa kwani wajasiriamali hao wana uhutaji mkubwa na wamekuwa wakitafuta huduma hiyo lakini wanashindwa kuwahudumia kutokana na kutokidhi vigezo.
“Tunashindwa kuwapatia mikopo kutokana na kushindwa kuweka mali yoyote kama dhamana endapo watashindwa kurejesha fedha,” amesema.