Imekuwa ni kawaida kuona kuwa mtu ameomba mkopo na kupewa majibu kuwa ‘hajakidhi vigezo’ vya mkopo hasa katika taasisi za fedha kama benki. Hii hutokana na kuwa na pointi chache za ukopaji (nikimaanisha si mkopaji aliyezoeleka hivyo benki haiwezi kumuamini mtu anayekopa kwa mara ya kwanza) au kipato kilichopo katika akaunti ya benki hakiridhishi kuchukua mkopo husika.
Ikiwa huna vigezo mara nyingi hutakiwa kutafuta wadhamini ili uweze kupata mkopo huo na ikiwa lolote litatokea basi mdhamini/wadhamini wako watachukua jukumu la kulipa mkopo huo. Ifahamike kuwa mkopeshaji atakubali kukopesha ikiwa mdhamini wako ana historia nzuri ya kukopa na ana kipato cha kueleweka.
Na ikiwa wewe na mdhamini wako mkashindwa kulipa mkopo huo basi mkopeshaji ana haki ya kuwapeleka katika vyombo husika vya sheria ili kuhakikisha fedha zake zinarudi. Hivyo basi ikiwa unahitajika kutafuta mdhamini hakikisha unatafuta mdhamini mwenye maslahi au tafuta njia nyingine kupata fedha hizo.
Pia ni vyema kuhakikisha mdhamini wako anajua hatari anayojihusisha nayo ikiwa wewe umepata tatizo lolote (kulipa mkopo wote), kwa sababu sio siku zote mambo yataenda sawa, majanga yanaweza kutokea muda wowote. Hivyo hakikisha anatambua hilo.
Hakikisha mdhamini wako ana nyaraka zote stahiki wakati anasaini nyaraka zinazohitajika ili uweze kupata mkopo. Kuwa na nyaraka ambazo hazijakamilika kutawapotezea muda na mkopeshaji ataona haupo makini na suala hilo. Hivyo hakikisha wote mna nyaraka zote stahiki.
Kuwa makini na mikopo inayohusisha uwekezaji wa mali (Collateral). Kila siku watu wanaondolewa katika nyumba zao, wananyang’anywa magari yao kwa sababu ya kukubali mkataba wa mkopo unaohusisha mali. Hivyo ni muhimu kutafakari, kufanya utafiti kuhusu mkopo unaofikiria kuomba, mahali unapotaka kuomba na namna utakavyolipa mkopo huo. Sio vyema maamuzi binafsi yawaumize watu wengi kama familia na mdhamini wako.