Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba ametoa wito kwa vyama vya ushirika hapa nchini kuwa na mazoea ya kukopa kwa niaba ya wanachama wao kwani wengi hawakopeshwi na mabenki, hali inayopelekea shughuli zao za kilimo kuwa ngumu. Mgumba amesema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na maofisa ushirika, kilimo na umwagiliaji na kuongeza kuwa, miundombinu ya umwagiliaji huhitaji marekebisho makubwa ili kutumika na wakulima.
Naibu Waziri Mgumba ameeleza kuwa miundombinu hiyo imekosa ukarabati kwa sababu wakulima hawana mitaji ya kutosha, jambo linalopekelea taasisi za fedha kutowaamini na hivyo kushindwa kuwasaidia na ukarabati huo. Ameagiza tume ya ushirika kuhakikisha inavisimamia vyama vya ushirika ili viweze kukopa fedha kwa ajili ya wanachama.
“Hatuwezi kufanya kilimo cha kibiashara kwa kutegemea mvua ambazo nazo zimekuwa hazitabiriki, nawashauri tume ya ushirika na tume umwagiliaji kusimamia vyama hivyo kwenye skimu mbalimbali za umwagiliaji kukopa fedha ambazo zitatumika kurekebisha miundombinu ya umwagiliaji badala ya kutegemea serikali”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Akichangia mjadala huo, Afisa umwagiliaji wa Kanda, Mhandisi Juma Mdete amesema ukanda huo una eneo la takribani hekta 40,000 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji lakini eneo linalotumika ni hekta 24,000 pekee.