Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ametoa wito kwa wajasiriamali walionufaika na mikopo ya Halmashauri kuhakikisha fedha wanazopata hazitumiki kwa matumizi binafsi na badala yake wazielekeza katika biashara zao ili kujikwamua kiuchumi. Wangabo amesema hayo wakati akikabidhi mikopo yenye thamani ya Shilingi 53 milioni, ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi 15 vya Halmashauri ya wilaya hiyo.
“Kwenye vikundi vyenu mna malengo mahususi na ili haya malengo mahususi yaweze kutimia kwenye biashara hakuna kingine zaidi ya kuwa bahili lazima muwe mabahili, lazima muwe watu ambao hamkubali kutoa fedha hovyo hovyo, usikibali kutoa fedha ambayo haina mpango, leo unaambiwa kuna msiba pale wewe unachukua fedha ya mkopo unapeleka, huu sio ubahili, weka fedha yako vizuri, kama kuna shida tafuta hela nyingine na ukichukua fedha inayotokana na hapo labda ni faida”. Amesema Mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emanuel Sekwao amesema kwa mwaka wa fedha 2018/2019, vikundi 15 viliwasilisha maombi ya mikopo ya Sh. 68,292,000.00. lakini baada ya Kamati ya Mikopo kupitia maombi hayo, Sh. 53,000,000 yalipitishwa.
“Vikundi vitakavyokopeshwa ni 15 ambapo vikundi vya vijana vitatu, jumla ya fedha Sh. 12,687,000, kikundi cha walemavu kimoja, jumla ya fedha Sh. 2,000,000 na vikundi vya wanawake kumi na moja, jumla ya fedha Sh. 38,313,000. Vikundi hivyo vimetoka katika kata za Mashete, Kipundu, Majengo, Sintali, Namanyere, Chala, Kipande, Kabwe, Kate, Kirando na Kala”. Amesema Kaimu huyo.