Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameshangazwa na kitendo cha wakulima mkoani Mbeya kusuasua kwenye uombaji mikopo japokuwa wanaongoza katika uzalishaji wa mazao mbalimbali. Rais Magufuli ametoa wito kwa wakulima mkoani humo kuwa mstari wa mbele na kuchangamkia mikopo ya riba nafuu inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na kusisitiza kuwa, benki hiyo imeanzishwa na serikali kwa ajili yao ili kutatua adha ya upatikanaji mitaji na vilevile kuinua kilimo.
“Mpaka Machi mwaka huu, TADB ambayo ni benki yenu nyinyi wakulima ilikuwa imeshatoa mikopo ya thamani ya Sh. 102 bilioni kwa wakulima nchi nzima ambapo wakulima Mbeya wamekopa Sh. 779.9 milioni tu. Tumeendelea kuimarisha Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo na sasa imeanza kutoa mikopo kwa wakulima. Na hii ndiyo fursa pekee kwenu kuchangamkia mikopo yenye riba nafuu. Fikiria wakulima wa mikoa ya Mtwara na Lindi wamekopa Sh. 33 bilioni ambapo Mwanza wamekopa Sh. Bilioni 11.2 na nyinyi Mbeya ambao ni wazalishaji wakubwa mmekopa pungufu ya Sh. Bilioni moja”. Ameeleza Rais Magufuli.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli pia ametumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa TADB kwa kuwahudumia wakulima huku akisisitiza kuwa wakulima wa Mbeya wanapaswa kuitumia benki hiyo ili kuchochea maendeleo kwenye sekta ya kilimo.