Home FEDHA Mitandao ya kijamii inavyoweza kuharibu bajeti yako

Mitandao ya kijamii inavyoweza kuharibu bajeti yako

0 comment 99 views

Katika miaka ya hivi karibuni kundi kubwa la watu hasa vijana wamekuwa wakitumia mitandao kama vile Facebook na Instagram kama mahali pa kuonyesha biashara, ubunifu na vipaji vyao kwa lengo la kujitangaza ili kupata wateja. Mitandao hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kwani imekuwa njia rahisi ya kujiingizia kipato. Lakini kwa upande wa pili, kuna kundi la watu ambao hujikuta wanatumia pesa zaidi kufanya manunuzi mtandaoni na hali hiyo inapelekea wao kuwa na matumizi mabaya ya fedha.

Ifahamike kuwa, wafanyabiashara wa mitandaoni wapo kwa dhumuni moja tu ambalo ni kutengeneza pesa. Wakati mwingine wanafanya kazi na wasanii au watu maarufu ambao ushawishi wao ni mkubwa katika jamiii ili kuwavuta zaidi wateja wao ili mradi tu wauze bidhaa zao. Watu wengine hushindwa kujizuia na kujikuta wakiingia gharama kubwa kununua bidhaa wanazoziona mtandaoni wakiamini kuwa wasipokuwa na bidhaa hiyo wanapitwa ama wanaonekana kama watu ambao hawaendi na wakati.

Ushawishi kutoka kwa marafiki pia inachangia kwa kiasi kikubwa katika hili. Vijana ndio waathirika wakubwa wa kufanya maamuzi yasiyo ya busara kifedha kutokana na ushawishi. Unajikuta unashawishika kununua vitu fulani mitandaoni au kwenda mahali fulani ambapo kwa mujibu wa mitandao ya kijamii ndio sehemu ya kijanja na bila kuangalia bajeti yako unatumia fedha nyingi kuliko kawaida. Vitendo kama hivi vinarudisha nyuma watu wengi na wanajikuta wanashindwa kutimiza malengo muhimu zaidi waliyonayo.

Mtu anayetumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kwa namna moja au nyingine hujikuta akitamani vitu au huduma fulani mara baada ya kuona kwa watu wengine. Hali hiyo ni ya kibinadamu na mara nyingi huwezi kuiepuka. Hii inakuja kama athari mojawapo ya kutumia mitandao kwa muda mrefu. Ni lazima kubadilika na kujifunza kutumia busara zaidi katika masuala haya kwani wafanyabiashara mitandaoni ni wengi na huwezi kuwamaliza wote. Tumia mitandao katika njia ambayo haitakusababishia hasara na kuharibu bajeti yako. Ni kweli kuwa kufanya manunuzi mtandaoni ni rahisi kwani unatumia muda mfupi kupata huduma lakini umakini unatakiwa ili kuhakikisha kuwa matumizi yako yanaendana na bajeti yako.

Mitandao ya kijamii ikitumika kistaarabu, inakuwa jukwaa zuri la kujifunza, kuwasiliana na kushauriana na watu mbalimbali, kupata elimu ya ujasiriamali na kujitangaza kwa watu. Kama jamii, ni vizuri tukatambua mchango mkubwa wa teknolojia katika maendeleo. Vijana wengi wameweza kutumia jukwaa la mitandao kujiingizia kipato hivyo uhamasishaji zaidi uendelee kutolewa ili kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya biashara na huduma mbalimbali. Wanunuzi nao wanatakiwa kuwa makini ili wasijikute wanatumia fedha kupita kiasi sababu ya biashara za mitandaoni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter