Meneja wa kiwanda cha UTT Njombe, Alawi Mdee amewaambia waandishi wa habari kuwa, kampuni ya muda mrefu ya kuzalisha majani ya chai nchini, Unilever (UTT) imewekeza takribani Sh. 18 bilioni kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kisasa cha uzalishaji wa majani ya chai mkoani humo.
Mdee amesema hayo kwa waandishi waliokuwa kwenye ziara wakijifunza mnyororo wa thamani wa zao hilo na kuongeza kuwa, kampuni hiyo inalenga kuwainua wakulima wa Njombe kama ilivyofanya kwa wale wa Mufindi.
“Jumla ya Sh. 18 bilioni zilitumika kujenga kiwanda cha UTT cha Njombe, kiwanda kilianza kufanya kazi Machi 2018…kitakuwa kinapokea asilimia 70 ya majani mabichi kutoka kwa wakulima wadogo. Tunataka kutumia uzoefu wa Mufindi kuboresha hali za wakulima wa Njombe”. Amefafanua Meneja huyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UTT Ashton Eastman amesema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na kampuni inayohusika na kuwahudumia wakulima wadogo wa Njombe (NOSC) ili kufanikisha mipango ya kampuni hiyo kuboresha kilimo cha wakulima hao.