Teknolojia mbalimbali zinaendelea kuboreshwa ili kurahisisha maisha ya binadamu. Benjamin Fernandes, ni mmoja wa watu mashuhuri ambao waliona changamoto zilizopo katika kufanya miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu na kuchukua fursa hiyo kuanzisha App inayojulikana kwa jina la NALA, ili kutuma na kupokea fedha.
NALA ni nini?
NALA ni App ya kufanya miamala kwa urahisi, uharaka na usalama zaidi bila kutumia mtandao. App hii humuwezesha mtu yoyote mwenye simu ya Android kutuma na kupokea fedha, kulipa bili mbalimbali, kununua vifurushi, kufanya manunuzi, kujua na kufuatilia historia ya matumizi yake kwa urahisi bila gharama yoyote.
Kupitia NALA, changamoto mbalimbali zimesuluhishwa ikiwa ni pamoja na suala la USSD, ambapo kawaida katika laini za simu mtu akiwa anafanya muamala hutakiwa kupitia vipengele mbalimbali, jambo ambalo husababisha watu kutumia muda mrefu kufanya muamala mmoja na muda mwingine muamala huo unaweza usikamilike au mtu anaweza kukosea hivyo kumlazimu kurudia tena.
Hivyo basi kupitia App hii, mtumiaji hufanya miamala kwa urahisi na haraka zaidi. Kwa mfano ukitaka kumtumia mtu fedha, unachotakiwa kufanya ni kufungua App na kubonyeza sehemu imeandikwa “send money”, kisha kuweka namba ya mtu unayemtumia , halafu utahitajika kuweka kiasi na kukamilisha muamala wako.
Vilevile, mtumiaji anaweza kutuma fedha kwa mtu ambaye hana programu hii katika simu yake. Na ikiwa mtumiaji hana salio basi anaweza kukamilisha muamala wake.Hakuna haja ya kutumia mtandao wakati miamala inafanyika. Aidha, mtumiaji hushauriwa kutengeneza PIN number (namba ya siri) mpya katika akaunti yake ili kuwa katika hali ya usalama zaidi.
Pamoja na hayo, ili kupata historia fupi ya miamala uliofanywa, lazima ukatwe kiasi kidogo cha fedha, na licha ya kukatwa fedha kidogo huwezi kupata miamala yote uliyofanya. Lakini kupitia NALA mtumiaji hupata historia ya miamala yake yote sehemu moja tena bila malipo yoyote.
Watanzania ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata changamoto pindi wanapotuma/kupokea fedha au kufanya malipo wameipokea NALA kwa mikono miwili kwani ni mfumo rahisi zaidi kutumia na hakuna gharama za ziada.
Umewahi kutumia NALA kufanya miamala?