Noti mpya za Tanzania zenye sahihi ya Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia Februari Mosi 2025.
Gavana Tutuba amesema hayo wakati akimkabidhi Dkt. Nchemba, noti kifani za shilingi elfu kumi, elfu Tano, Elfu Mbili na Shilingi Elfu moja, katika Ofisi ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
“Mheshimiwa Waziri, ninayofuraha kukujulisha kuwa zoezi letu la uchapaji upya wa noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la Serikali” amesema Gavana Tutuba.
Gavana Tutuba amefafanua kuwa Noti hizo zitatumika sambamba na noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa Noti zilizotolewa Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye sahihi ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa BoT.
“Sahihi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango imebadilishwa na kuwekwa sahihi yako Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na sahihi ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa sahihi ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Emmanuel Tutuba,” amebainisha Gavana huyo.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya, Dkt. Nchemba amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa BoT kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,” amesema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliridhia noti hizo ziingizwe kwenye mzunguko na kuanza kutumika kama ilivyopangwa tarehe moja Februari mwaka huu.