Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Ashatu Kijaji amesema kuwa marekebisho ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2018 hayalengi kuzuia watu, taasisi au vyuo kufanya utafiti bali madhumuni makubwa ya marekebisho na uridhiaji wa Mkataba wa Takwimu wa Afrika ni kuhakikisha takwimu zinazozalishwa zinazingatia viwango. Dk.Kijaji ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya takwimu Afrika.
“Niwatoe wasiwasi wananchi na wadau mbalimbali kwamba marekebisho haya yana lengo jema na hayana lengo la kuzuia kufanya tafiti”. Amesema Dk. Kijaji.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema wizara hiyo ipo katika mchakato wa kuandaa kanuni za utekelezaji wa marekebisho hayo na wadau mbalimbali watashirikishwa ili kuwe na uelewa wa pamoja wakati Sheria hiyo inatekelezwa kwa maslahi ya taifa.