Home FEDHA Tanzania inahitaji dola za Marekani bilioni 6.3 kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa

Tanzania inahitaji dola za Marekani bilioni 6.3 kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa

0 comment 51 views

Tanzania inahitaji dola za Marekani bilioni 6.3 kwa mwaka ili kukabiliana na athari za papo kwa hapo zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hayo wakati akizindua rasmi Ripoti ya Mapitio ya Hali ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2024, iliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Dkt. Nchemba ametaja mabadiliko ya hali ya hewa kuwa miongoni mwa eneo linalokwamisha maendeleo ya nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania.

Dkt. Nchemba amezindua Ripoti hiyo kwa njia ya mtandao akiwa Abuja nchini Nigeria, ambako anaongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mikutano ya Nchi za Afrika (African Caucus Meetings), wanachama wa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii na kuwa kinara miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, licha ya changamoto zinazoikabili Dunia ikiwemo athari za UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na mizozo ya vita inayoendelea maeneo mbalimbali duniani.

Dkt. Nchemba amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uchumi wake kupitia Mpango wake wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III), wenye lengo la kujenga uchumi imara, shirikishi na wenye ushindani kupitia sekta za uzalishaji, ikiwemo kilimo, uzalishaji viwandani, kuongeza thamani ya bidhaa, uwekezaji na biashara pamoja na kukuza ajira kwa wananchi hususan vijana.

Amezitaka Taasisi za Fedha za Kimataifa, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuweka mazingira ya upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu ili kuziwezesha nchi za Afrika kuwa na uwezo endelevu wa kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ajili ya nchi zao.

Ripoti hiyo ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania iliyowasilishwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika na unatarajia kupanda kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023, hadi asilimia 5.7 mwaka 2024, na utafika asilimia 6 mwaka 2025.

Ripoti hiyo imebeba kauli mbiu isemayo “Driving Tanzania’s Transformation – The Reform of the Global Financial Architecture”.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter