Home FEDHA Tanzania kukopeshwa bilioni 979

Tanzania kukopeshwa bilioni 979

0 comment 116 views

Tanzania imeahidiwa kupewa mkopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoa katika mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Miongoni mwa miradi itakayonufaika ni mradi wa umeme wa Benaco-Kyaka mkoani Kagera na ujenzi wa makazi ya watumishi ya gharama nafuu Zanzibar, inayokadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 420 sawa na Sh 979,374,404,740 za Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Mohammed Saif Al Suwaidi alitoa ahadi hiyo alipokutana na kuzungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba katika makao makuu ya mfuko huo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Suwaidi alisema miradi mingine ya kimkakati iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania kwenye mfuko huo ikiwamo ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Reli ya Kisasa (SGR), itatafutiwa ufadhili kupitia serikali na sekta binafsi ya nchi hizo.

Alisema mfuko huo uko tayari kusaidia pia utekelezaji wa miradi mingine ya kilimo na uvuvi, na fedha hizo zitapatikana kupitia kampuni inayojishughulisha na masuala hayo katika Serikali ya UAE.

Dk Mwigulu alikumbushia upatikanaji wa fedha za miradi sita iliyowasilishwa na serikali katika mfuko huo ikiwamo SGR kutoka Tabora-Kigoma-Msongati, ujenzi wa JNHPP, Mradi wa Umeme wa Benaco hadi Kyaka (kilovolti 220), mradi wa kuwezesha biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa kutoka nje na ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi nafuu Zanzibar.

Aliushukuru mfuko huo kwa kutoa Sh milioni 201 na dola za Marekani milioni 1.3 za Mradi wa Barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami, barabara ambayo ujenzi wake umerejea baada ya kukwama kwa muda mrefu.

Naibu Katibu Mkuu Hazina, Lawrence Mafuru alisema ahadi hiyo ni matunda ya kusainiwa kwa mkataba wa kutotoza kodi mara mbili kwenye mapato ya faida pamoja na udhibiti wa ukwepaji kodi uliosainiwa juzi kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu mjini Dubai.

Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi umetoa fedha za utekelezaji wa miradi nchini ukiwamo ujenzi wa Hospitali ya Wete Pemba, Barabara ya Kidawe hadi Uvinza, ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera na Mradi wa Maji Zanzibar Vijijini iliyokamilika na sasa wanafadhili ujenzi wa Barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter