Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), imewahakikishia walipakodi nchini kuwa itashughulikia malalamiko ya wafanyabiashara yanayohusiana na kodi kwa haki na usawa ili kuchochea ulipaji kodi kwa hiyari.
Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Robert Manyama ameleza hayo alipokutana na wadau wa kodi jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, wakati akitambulisha malengo ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo iliyoanza rasmi kutekeleza majukumu yake.
Amesema Taasisi hiyo imeundwa na Serikali, chini ya Wizara ya Fedha, ikiwa ni Taasisi huru itakayokuwa na jukumu la kutoa usuluhishi wa malalamiko baina ya walipa kodi na watozakodi (Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA) ili kupunguza malalamiko ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu na kuwa kikwazo kwa ulipaji kodi wa hiyari.
‘‘Tunatoa uwanja huru wa mlipakodi kupata haki yake bila kuona kuwa anayetoa usuluhishi wa malalamiko yake ni yuleyule aliyesababisha kutokea kwa malalamiko, lakini pia nitoe wito kwa wafanyabiashara wajitahidi kutunza kumbukumbu za biashara kwa usahihi ili kupata suluhu kwa kuzingatia ukweli na haki’’, amesema Manyama.
Ameeleza kuwa haki inaambatana na wajibu hivyo wafanyabiashara ni vema kutekeleza wajibu wao wakati Taasisi ikiwa inashugulikia malalamiko yao kwa kutoa ushirikiano wakati wanapohitajika kutoa taarifa fulani ili kuwezesha mchakato kufanyika ndani ya muda uliowekwa.
Manyama amesema Taasisi hiyo pia katika kuzuia malalamiko inaendelea kutambua matatizo yaliyo ndani ya mfumo wa kodi yanayosababisha migogoro na kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mapendekezo ili kufanyike marekebidho ndani ya mfumo wa kodi.
“Tutashughulikia malalamiko kama yalivyo ila nasisitiza tuwe wakweli tukiwa wakweli tutatatua malalamiko, na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kupita mikoani ili kuweza kuwafikia katika maeneo yao,” ameeleza.
Amebainisha kuwa Taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kuwa hakuna namna itaingiliana na majukumu ya Taasisi nyingine ya Serikali na kuwa Sheria iliyounda TOST imeipa uhuru wa kutokuingiliwa na Taasisi nyingine kiutendaji.