Home FEDHA Unataka kujiendeleza? Epuka haya

Unataka kujiendeleza? Epuka haya

0 comment 93 views

Kila siku unaweza kuwa unajiuliza kuwa fedha zako unazopata zinaishia wapi, na kwanini kila baada ya muda unakuwa huna fedha hivyo kusababisha shughuli zako kutoendelea. Watu huwa na kawaida ya kupuuzia mambo mengi hasa yanayohusu fedha kwa sababu wamejiwekea mtizamo kuwa fedha zinatafutwa hata kama zikiisha leo basi kesho zitatafutwa na maisha yataendeea. Hii sio sahihi kama unataka kuendelea na kufanya maendeleo.

Hivyo imefika wakati muafaka wa kuachana na mambo yafuatayo ili kuleta mabadliko hasa katika upande wa fedha na maendeleo.

Kukosa Mipango

Maendeleo ya baadae hasa katika uchumi hutegemeana na mipango inayopangwa sasa. Kama huna mipango basi usitegemee mabadiliko baadae. Ndio maana unashauriwa kuanza kujiwekea mipango na kujua jinsi utakavyoitekeleza mipango hiyo. Kuna mipango ya muda mfupi na ya muda mrefu hivyo angalia kipato chako halafu kigawanyishe kwenye matumizi yako ya kila siku, katika mipango ya muda mfupi vilevile na kwenye mipango ya muda mrefu. Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kujua muelekeo wako na wapi umefikia, mambo yapi uyabadilishe ili kuhakikisha mambo yanakwenda na mabadiliko yanaonekana.

Kutowekeza

Kwanza ifahamike kuwa sio kila mtu anatakiwa kuwekeza katika biashara au ujasiriamali. Kuna fursa nyingi ambazo mtu anaweza kuwekeza na kunufaika. Hivyo anza sasa kufikiria kama wewe unafaa kuwa mjasiriamali, mfanyabiashara au kama uwekezaji katika sekta ambazo zinaweza kukuletea maendeleo. Chukua muda wako, usiige watu wengine kwani kufanya hivyo si sahihi na kunaweza kupata hasara na kurudi nyuma.

Kulipa madeni na akiba

Sio vibaya kukopa lakini jambo la muhimu unalotakiwa kuanza kufanya kila ukikopa ni kufikiria njia ambayo itarudisha mkopo huo ili kuepuka kutumia fedha unazoweka akiba kulipa mikopo. Ikiwa imeshindikana kabisa kupata fedha kulipa mkopo na njia iliyobaki kulipa mkopo huo ni kupitia akiba unazojiwekea basi hakikisha unarudisha fedha ulizochukua katika akiba yako ili mambo yaende sawa.

Matumizi mabaya ya fedha

Kuna matumizi ya muhimu kama kodi ya nyumba, chakula n.k na kuna vitu ambavyo mtu hutamani lakini si vya muhimu na hata akifanikiwa kuvipata hakuna faida yoyote atakayopata zaidi ya kuridhika na kujulikana kuwa anavimiliki. Sio mbaya kutumia fedha katika mambo hayo lakini usijiwekee mazoea ya kununua vitu visivyo na umuhimu ili hali kipato chako hakiruhusu na hata kama kinaruhusu basi wekeza fedha hizo katika mambo mengine ya muhimu. Kwa mfano ikiwa ni lazima kununua gari basi nunua gari linaloendana na bajeti yako ili kuepuka kutumia fedha nyingi kuweka mafuta, kufanya marekebisho na mambo mengine na mwisho wa siku kuharibu bajeti yako.

Kutumia mshahara wote

Hili ni tatizo kwa watu wengi,na mtu hawezi kuona kuwa hili ni tatizo hadi pale atakapopata matatizo na kushindwa kutatua tatizo hilo au pale muda wa kulipwa utakapofika na mwajiri asitoe fedha kwa muda muafaka. Hivyo ifike wakati watu waanze kuweka akiba ili kuepuka usumbufu pale fedha zinapohitajika.

Si rahisi kubadilika ndani ya siku moja, lakini kwa kuanza, kuwa makini katika matumizi madogo hii itakusaidia baadae kuweza kumudu fedha unazotumia katika matumizi makubwa pia jambo la msingi ni kuweka akiba kwa ajili ya baadae.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter