Mitandao ya kijamii kama Instagram na Facebook ni miongoni wa sehemu ambazo ambazo siku za hivi karibuni, watu wengi wamekuwa wakiendelea kutengeneza fedha kwa njia mbalimbali. Ikiwa wewe ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii, hata wewe unaweza kuitumia kujiajiri na kuingiza kipato cha uhakika ikiwa unajua nini hasa wafuatiliaji wako wanahitaji na kitu gani kinakosekana katika soko.
Lakini unawezaje kupata fedha kwenye mitandao ya kijamii? Unafahamu unachotakiwa kufanya? Ni mambo gani unapaswa kuzingatia?
Hatua zifuatazo ni mwanzo mzuri wa kufanikisha hilo.
- Wachukulie wafuatiliaji wako kama marafiki
Mara nyingi, watu wanadhani kwamba unahitaji mamilioni ya wafuatiliaji ili kutengeneza fedha mtandaoni lakini sio kweli. Unaweza kuingiza fedha nzuri tu hata kama una wafuatiliaji 100, lakini umejenga mahusiano mazuri. Ni rahisi sana kupoteza muelekeo kutokana na masuala ya idadi ya wafuatiliaji lakini unachotakiwa kukumbuka ni kwamba wafuatiliaji sio namba, ni watu. Unapowachukulia wafuatiliaji wako kama watu wa kawaida na marafiki, basi ni rahisi kutengeneza fedha. Hakikisha unawatumia kauli nzuri, unawajibu pale wanapouliza maswali na unafuatilia kurasa zao pia.
- Fahamu wafuatiliaji wako wanahitaji nini
Ni muhimu kutumia mitandao ya kijamii kuzungumza na wafuatiliaji wako na kufahamu kutoka kwao, ni nini hasa wanahitaji au wanapendelea. Unaweza kuuliza maswali na kupitia majibu yao, inakuwa rahisi zaidi kujua wanakosa nini kwa wakati huo. Baada ya kufahamu wanachohitaji, unaweza kuwapa bidhaa au huduma itakayotatua changamoto waliyonayo. Unapofahamu nini hasa wanahitaji, unajua nini hasa unatakiwa kuwapatia.
- Fanya utafiti wa soko
Bila shaka, tayari kuna mamia ya akaunti ya Instagram na Facebook ambayo tayari yanafanya unachofikiria kufanya. Hii sio sababu ya kukata tamaa. Unatakiwa kufanya utafiti wa kutosha ili kuelewa soko, kujua wateja wanachohitaji na vilevile kufahamu washindano wako. Unapofanya utafiti unapata uelewa wa vitu vya msingi kama vile muda gani unatakiwa kuwa mtandaoni, jinsi ya kuongea na wateja wako n.k. Badala ya kukimbia kuanzisha biashara, wekeza muda wa kutosha kuelewa soko na kuwa na mikakati ya kuvutia wateja.