Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule kuwakamata viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa Dola 21,000 za Marekani. Majaliwa ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha kangeme wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Kamanda Haule amewataja watuhumiwa kuwa ni Mwenyekiti, Shilinde Abdallah, Mhasibu wa chama hicho, Kulwa Shinzi na wajumbe saba wa bodi ya chama. Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU), Emmanuel Cherehani amesoma taarifa na kusema kuwa, bei ya tumbaku ni nzuri, lakini wananchi walimzomea kuonyesha hali ya kupinga juu ya kile alichokisema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amesema kuna tatizo la upangaji madaraja kwa kuwa wakulima wanalima tumbaku nzuri, lakini katika upangaji bei wakulima wanalipwa fedha kidogo. Dk. Tizeba amedai kuna wakulima wanakidai Chama cha Msingi cha Mkombozi madai ya tumbaku waliyouza tangu mwaka 2014.