Home KILIMO Njia za uzalishaji bora wa tangawizi

Njia za uzalishaji bora wa tangawizi

0 comment 40 views

Tangawizi ni moja kati ya mazao ya viungo yanayozalishwa katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo zile za ukanda wa Afrika Mashariki. Zao la tangawizi lina faida nyingi za kiafya sambamba na kuongezeka kwa matumizi yake katika shughuli za usindikaji wa vinywaji kama vile, juisi na soda pamoja na kutebngeneza dawa za binadamu viwandani.

Mambo ya kuzingatia katika kilimo cha tangawizi

  1. Udongo na kustawi

Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha milimita 1,200-1,800 na joto la wastani wa nyuzi joto 20°C-25°C. Tangawizi hustawi vema katika udongo tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.

  1. Aina za Tangawizi

Mpaka hivi sasa hakuna aina rasmi za tangawizi ambazo zimeainishwa na kuthibitishwa kuzalishwa nchini Tanzania. Pamoja na hili, kuna aina tatu za tangawizi ambazo zimezoeleka kuzalishwa na wakulima hapa nchini. Aina hizo ni tangawizi nyeupe maarufu kama,White Africa au  Jamaica, Cochin (Flint), na Bombay. Tangawizi inayopandwa katika sehemu tambarare huwa laini zaidi kuliko inayozalishwa kwenye maeneo ya milima, ambayo huwa ngumu na kuwa na nyuzi nyingi zaidi.

  1. Nafasi

Nafasi inayotumika kupanda ni kati ya sentimita 23-30 kwa 15-23 na kina cha sentimita 5-10. Unaweza kupanda sehemu yenye miti au migomba ili kuweka kivuli chepesi ingawa si lazima kivuli kiwepo. Inashauriwa kumwagilia maji mara kwa mara endapo mvua inakosekana hadi kufikia mwezi mmoja kabla ya kuvuna.

Tangawizi pia hutumika  katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi. Hali kadhalika tangawizi hutumika katika kutengeneza vipodozi vya aina mbalimbali vile kama poda

  1. Mbegu na namna ya kupanda

Zao la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu. Vipande vya tangawizi huhifadhiwa mahali pakavu penye ubaridi ili kuweza kuchipua. Machipukizi hukatwa urefu wa sen-timita 2.5-5. Baada ya hapo, unaweza kupanda machipukizi hayo kwenye matuta au shambani kawaida endapo eneo lako ni tambarare. Baada ya kupanda, tandaza nyasi shambani kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapokosekana.

  1. Matayarisho

Ondoa takataka zisizohitajika shambani. Wiki 1-2 kabla ya kupanda weka mbolea ya samadi au mboji kiasi cha tani 25-30 kwa hekari moja.

  1. Palizi

Katika kipindi cha wiki mbili, magugu huanza kuchomoza kwa kuwa udongo huwa na unyevu kwa wingi. Fanya palizi mara majani yanapojitokeza. Endelea kung’oa magugu na kuweka shamba katika hali ya usafi hadi wakatiwa kuvuna.

  1. Kupanda

Tangawizi ni mmea unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu ya ardhi. Jamaica ina rangi hafifu ya kahawia na tunguu fupi wakati Cochin ina tunguu fupi zaidi lenye ngozi ya rangi iliyo kati ya kijivu na nyekundu. Mmea una urefu wa futi mbili na majani yake ni membamba marefu, ambayo hufa kila mwaka yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua ya mmea huu yana rangi nyeupe au manjano.

  1. Magonjwa na wadudu

Madoa ya majani-Yanayosababishwa na viini vya magonjwa viitwavyo Colletotrichum zingiberis na Phyllosticta zingiberi.

Kuoza kwa tunguu-Kunasababishwa na viini viitwavyo Pithium spp.

Mizizi fundo-Inasababishwa na meloidegyne spp.

  1. Uvunaji

Tangawizi huweza kuwa tayari kwa kuvuna kati ya miezi 9-10 baada ya kupanda, wakati majani yake yanapogeuka rangi kuwa njano na mashina kusinyaa. Tangawizi itakayohifadhiwa ivunwe mapema kabla haijakomaa kabisa, na ile iliyokomaa kabisa huwa kali zaidi na huwa na nyuzi hivyo hufaa kwa kukausha na kusaga. Mavuno hutofautiana kulingana na huduma ya zao, yanaweza kuwa kiasi cha tani 20-30 cha tangawizi mbichi huweza kupatikana kwa hekari moja.

  1. Soko la tangawizi

Soko la tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi kikubwa kinauzwa nchini. Bei yake ni kati Sh. 300-1,500/- kwa kilo moja kutegemeana na msimu.

 

Tangawizi hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji kama vile chai, soda, juisi, vilevi na kadhalika. Kuna aina mbalimbali za vyakula ambavyo pia hutengenezwa kwa kutumia tangawizi kama vile mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga, achari na kadhalika. Tangawizi pia imekuwa ikitumika katika viwanda mbalimbali kwa ajili ya kuzalisha dawa za binadamu.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter