Wakati wa kuchangia hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/2020, baadhi ya wabunge wameshauri Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) kuongezewa fedha kutoka asilimia 30 hadi asilimia 50 ili kuiwezesha kufanya maboresho zaidi, hasa katika mtandao wa barabara za vijijini.
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli amesema kutokana na Tarura kuwa na mtandao mkubwa wa barabara wa kilomita 130,000 tofauti na Tanroads ambayo ina kilomita 30,000, kuna kila sababu ya serikali kuwaongezea Tarura fedha .
“Naomba nishauri serikali waweze kubadili Sheria ili watu wa Tarura waweze kuongezewa fedha, Dar es salaam tuna matatizo makubwa ya barabara, ukiangalia jimbo la Segerea tuna barabara moja ya lami iko kata ya Kimanga, hivi sasa inajengwa kwa muda wa miaka minne kutokana na tatizo la bajeti”. Amesema Kamoli.
Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage amesema ili kurahisisha shughuli za ujenzi wa barabara vijijini, ingefaa kuanzishwa mfuko wa barabara ambao utashughulikia masuala ya ujenzi wa mtandao wa barabara za vijijini. Kwa upande wake, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mahamoud Mgimwa amesema changamoto ya barabara ipo vijijini zaidi na kama mabadiliko ya asilimia 50-50 hayatofanyika, shughuli za usafirishaji wa malighafi na mazao kutoka vijijini zitakwama.