Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha yamelenga kuwawezesha wananchi kupata uelewa wa masuala ya fedha.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wasimamizi wa Sekta ya Fedha nchini, wameandaa maadhimisho hayo ambayo Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Ruanda-nzovwe Jijini Mbeya.
Maadhimisho hayo yanalenga kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu matumizi ya huduma rasmi za fedha ambapo Serikali inakusudia takribani asilimia 80 ya wananchi watakuwa wamepata uelewa wa masuala ya fedha ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishina Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha Janeth Hiza amesema maadhimisho hayo pia yanalenga kuongeza mchango wa Sekta ya Fedha kwenye ukuaji wa uchumi.
Amesema kwa mujibu wa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 nchini, ni asilimia 53.5 tu ya nguvu kazi ndiyo wanaotumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la Watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo.
“Kutotumia huduma rasmi za fedha kunasababisha wananchi kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza Pato la Taifa”, amebainisha Hiza.
Ameeleza kuwa katika maadhimisho hayo wananchi watapatiwa elimu kuhusu faida ya kutumia huduma rasmi za fedha, usimamizi wa fedha binafsi katika utumiaji, uwekaji akiba pamoja na haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma za fedha.
Hiza amesema pamoja na kutoa elimu kwa wananchi, pia watatoa elimu hiyo kwa wanafunzi ili waweze kujua umuhimu wa kutumia huduma za fedha wakiwa wadogo tofauti na ilivyo hivi sasa.
Amesema kuwa utamaduni huo ukijengwa katika ngazi hiyo ya chini uelewa unaweza kuwa mkubwa na faida kwa nchi kwani vijana wadogo wanaweza kutumia na kujua umuhimu wake wakiwa vijana.
Kwa upande wao Wasimamzi wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) na Hifadhi ya Jamii wamewakaribisha wananchi kushiriki Maonesho hayo muhimu.
Wamesema kutembelea maadhimisho hayo hawapati tu elimu bali na huduma zote zinazotolewa na taasisi hizo zinazopatikana katika viwanja hivyo.
Maadhimisho hayo yanafanyika kuanzia Oktoba 21 hadi 26, 2024.