Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inatarajia kutoa Sh. 27.4 bilioni za Kenya (Sawa na Euro 235 milioni) kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la umeme la Thwake, lililopo mto wa Thwake kusini mwa nchi hiyo. Mradi huo ambao ni mkubwa zaidi kufadhiliwa na AfDB nchini Kenya unajumuisha kusambaza maji katika maeneo yaliyozunguka mradi huo ikiwa ni pamoja na mji wa teknolojia wa Konza. Kati ya fedha hizo, Euro 192.5 milioni zitatolewa na Benki ya Maendeleo huku Euro 43 milioni zikitoka katika Mfuko wa Afrika Ikue Pamoja (AGTF).
Taarifa rasmi ya serikali ya Kenya imeeleza kuwa, maji mililita za ujazo 22 milioni zitatumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji huku mililita za ujazo 34 milioni zitaelekezwa kwa ajili ya matumizi ya myumbani. Mara baada ya ujenzi wa bwawa hilo lenye urefu wa mita 80.5 kukamilika, maji kiasi cha mililita za ujazo 681 milioni yatakayotumika katika uzalishaji wa umeme na kilimo yataweza kuhifadhiwa. Bwawa hilo linatarajiwa kujengwa kwa awamu tatu na awamu ya mwisho inatarajiwa kukamilika Desemba 2022.