Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli anatarajia kuwaongoza watanzania katika mapokezi ya ndege mpya ya Airbus A220-300 itakayowasili leo majira ya saa sita mchana ikitokea nchini Canada. Ujio wa ndege hiyo ni muendelezo wa jitihada zinazofanywa na serikali kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameeleza kuwa, ujio wa ndege hiyo umetokana na ahadi za Rais Magufuli za kulifufua upya Shirika la Ndege.
“Pamoja na changamoto zote za kupingwa, lakini mwanaume huyu (Magufuli) amekuwa shupavu kapambana na kesho (yaani leo) inatua Airbus ya pili ikiwa ni kati ya zile ndege mbili kubwa alizoziagiza kati ya ndege saba zinazopaswa kuletwa kwa ajili ya Shirika letu la ndege”. Amesema RC Makonda.
Aidha, Makonda ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kuungana na Rais Magufuli katika hafla ya mapokezi itakayofanyika kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA).