Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Kitengo cha huduma kwa wateja kiboreshwe

Kitengo cha huduma kwa wateja kiboreshwe

0 comment 125 views

Ukizungumzia masuala ya huduma kwa wateja, taasisi nyingi za hapa nchini bado zina changamoto kubwa katika sekta hii. Makampuni ya mawasiliano ya simu, benki pamoja na mashirika mengine ya serikali na yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakilalamikiwa na watu wengi katika masuala ya kutoa huduma bora kwa wateja. Inaaminika kuwa asilimia kubwa ya walioajiriwa katika sekta hii hawana elimu, ujuzi wala mafunzo ya kutosha kuhusiana na kutoa huduma bora hivyo wanashindwa kufanya kazi zao kama inavyotakiwa.

Kitengo cha huduma kwa wateja ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya taasisi yoyote. Wateja au wawekezaji wanapofika katika sehemu hizi wanakutana kwanza na watoa huduma hawa hivyo wanabeba jukumu kubwa sana la kutangaza vyema taasisi wanazofanyia kazi. Kumekuwa na malalamiko kutoka sehemu nyingi kuwa vitengo vya huduma kwa wateja vimekuwa vibovu na huduma zao kwa kiasi kikubwa haziridishi. Hivyo basi taasisi husika zinachukua hatua gani ukabiliana na tatizo hili? Kwanini wanaoajiriwa katika kitengo hiki hawafanyi kile walichoajiriwa kufanya?

Inawezekana suala la elimu likawa changamoto kubwa katika sekta hii. Watu wengi wanaoajiriwa ili kutoa huduma kwa wateja hawana historia ya kusomea tasnia hiyo, hawana maarifa ya kutosha hivyo wanashindwa kuwahudumia wateja kama inavyotakiwa na pia wanakosa mafunzo ya kutosha kufahamu namna taasisi husika inawasaidia wateja wake. Lakini basi ni kwanini wanaajiriwa licha ya kuwa hawana vigezo vya nafasi hizo? Ni kweli baadhi ya wakuu katika sehemu hizi huwapatia tu kazi watu hawa kiholela kwa sababu ni ndugu au marafiki wa karibu?

Kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha vitengo vya huduma kwa wateja hapa nchini. Bila ya kuwa na huduma bora kwa wateja ni nani atahitaji huduma katika shirika hilo? Wateja hawataendelea kuwa wateja kama hawaridishwi na mwenendo mzima wa jinsi huduma zinavyotolewa. Inatakiwa kuwe na mfumo mzuri na unaoeleweka katika utoaji huduma ili kumshawishi mteja arudi tena siku nyingine.

Wafanyakazi katika kitengo hiki wanao wajibu wa kuhudumia wateja na kutatua matatizo yao kikamilifu bila usumbufu wowote. Hupaswi kutumia lugha ambayo sio nzuri na ni jukumu lako kutuliza wateja endapo hawatokuwa waelewa. Taasisi pia zinatakiwa kuhakikisha kuwa zinaajiri watu ambao wanakidhi vigezo vinavyotakiwa na kuwapa mafunzo ya kutosha kabla ya kuwaingiza kazini. Wateja wanayo haki ya kutoa maoni yao pale huduma wanayohitaji ikiwa na tatizo lolote na watoa huduma kwa wateja wanabeba jukumu la kuwasikiliza na kuondoa kikwazo chochote.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter