Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara nchini Kenya Chris Kiptoo amesema endapo hakutokuwa na mabadiliko ndani ya mwezi mmoja ujao, nchi hiyo itaanza kutoza ushuru kwa bidhaa za Tanzania na Uganda. Kenya imetangaza kufanya hivyo baada ya mvutano wa miezi kadhaa kuhusu bidhaa zake kutozwa ushuru mkubwa kinyume na mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Kuanzia mwezi wa tatu mwaka huu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) zimekuwa zikitoza bidhaa tamu kutoka Kenya kama vile pipi na juisi ushuru wa asilimia 25.
Kiptoo ameeleza kuwa watafanya maamuzi rasmi baada ya timu ya wataalamu wao kudhibitisha kama bidhaa hizo zinatumia sukari ya viwandani ili kujiridhisha.
Kufuatia maamuzi hayo, Sekretarieti ya EAC imepewa jukumu la kusimamia mchakato wa kudhibitisha malighafi inayotumika katika utengenezaji wa bidhaa ambazo zimekuwa zikilalamikiwa ambapo watahusisha pia bidhaa nyingine kama vile vipodozi, saruji, vilainishi vya mitambo pamoja na bidhaa za mbao ambazo zimekuwa zikipata vikwazo mara kwa mara kuingia Tanzania.