Home WANAWAKE NA MAENDELEO Wanawake wapanga mikakati kuwapiku wanaume

Wanawake wapanga mikakati kuwapiku wanaume

0 comment 34 views

Kumekuwa na malalamiko kwa muda mrefu sasa kuwa hakuna usawa wa kijinsia nchini. Tatizo hili sio la hapa kwetu pekee bali lipo katika mataifa mengi duniani. Wanawake hawapewi vipaumbele na kuwekwa mstari wa mbele kama ilivyo kwa wanaume katika sekta mbalimbali za maendeleo. Makundi na taasisi mbalimbali zimejitokeza kukemea ubaguzi wa kijinsia lakini bado kuna changamoto kubwa katika kutatua tatizo hili sugu.

Swali la kujiuliza hapa ni, kwanini jamii inafikiria ni sawa kumuweka mwanamke katika ngazi ya chini na kuamini kuwa wanaume ndio watawala? Chimbuko hasa la imani au fikira hii ni nini? Kwanini wanawake hawahusishwi na kushirikishwa katika sekta muhimu za kukuza uchumi sawa na wanaume?

Wanawake hasa wa vijijini wanaachwa nyuma kimaendeleo. Mwezi Mei mwaka jana, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) lilisema katika moja ya taarifa zake kuwa, inasikitisha na kufadhaisha kuona ukosefu wa usawa wa kijinsia barani Afrika. Shirika hilo lilisisitiza kuwa katika kundi hilo, wanawake ni wengi. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake wasiojua kusoma na kuandika ipo juu zaidi kulinganisha na ile ya wanaume.

Ni muhimu kujiuliza je hatua gani zinachukuliwa hapa nchini ili kupambana na hali hii? Serikali inatengeneza njia ili kuhakikisha wanawake wana haki sawa kama wanaume? Kisheria, kuna hatua zozote zinazochukuliwa ili kuhakikisha wanaotekeleza vitendo hivi vya kibaguzi wanaadhibiwa? Watoto wetu wanafundishwa kuanzia ngazi ya familia kuwa wanawake na wanaume wote ni sawa? Haya ni baadhi ya maswali muhimu ya kujiuliza.

Takwimu za Jukwaa la Uchumi Duniani zinaonyesha kuwa wanawake wengi hunyimwa nafasi za kazi katika idara mbalimbali japokuwa vyeti vyao huonyesha wana elimu sawa na wanaume. Katika takwimu hizo pia, inaonekana wanawake hupata fursa finyu za kiuchumi na kibiashara huku wanaume wengi wakipata fursa hizi kwa uraisi zaidi.

Ni wakati sasa wa wanawake kupigania usawa na kuacha kulalamika bila ya kuchukua hatua zozote. Wanawake wanapaswa kujituma zaidi na kulenga mambo makubwa wawapo katika mahala pao pa kazi. Uonevu huu hautafika mwisho kama wanawake wenyewe hawatakuwa mstari wa mbele kuulaani na kuukemea. Ni wakati wa kuonyesha jamii kuwa wao pia wanaweza na hawatokaa kimya pale ambapo wanaona wanaonewa na kunyimwa haki zao za msingi kwa kisingizio cha kwamba wao sio wanaume.

Serikali nayo ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki kwa wanawake. Viongozi wa kike nao watumie sauti waliyonayo kukemea ubaguzi wa kijinsia na pia watumie nguvu yao kuinua wanawake na watoto wa kike kwa ujumla. Changamoto hii ipo kwa kiasi kikubwa hapa nchini lakini wanawake wakiungana na kupiga vita tatizo hili kwa umoja, basi bila shaka watapiga hatua.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter