Siku chache baada ya Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango kuwasilisha mapendekezo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 bungeni Dodoma, wazalishaji wa pombe kali wameibuka na kudai wamefurahishwa na bajeti pamoja na mapendekezo kwani mfumo mpya wa stempu za kodi za kielektroniki utasaidia kumaliza tatizo la uwepo wa bidhaa bandia ambalo limekuwa kero kwa wazalishaji hao kwa muda mrefu.
Mojawapo kati ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Dk. Mpango ni pamoja na kuanzisha mfumo mpya wa stempu za kodi za kielektroniki ifikapo Septemba mwaka huu. Kwa mujibu wa maelezo aliyotoa Waziri huyo, mfumo huo mpya utawezesha serikali kutumia teknolojia ili kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani huku uvujaji wa mapato nao ukidhibitiwa.
Mbali na hayo, mfumo huo pia utasaidia kudhibiti tatizo la stempu za karatasi za kughushi, kitendo ambacho kimewapa faraja wazalishaji wa vinywaji vikali ambao wamedai kuwa mbali na kupata hasara, stempu hizo pia zimechangia kwa kiasi kikubwa kukosesha serikali mapato stahiki na kuchafua jina la soko hilo.