Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema kuanzia leo Jumatano Juni 23, 2021 mtu yeyote hatoruhusiwa kuingia eneo la hospitali au kutoa huduma bila kuvaa barakoa.
Pia mgonjwa atatakiwa kuwa na msindikizaji mmoja tu tofauti na hapo awali.
Taarifa iliyotolewa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma wa MNH, Amaniel Aligaesha inaeleza kuwa hatua hizo zinatokana na maagizo ya waziri wa afya kwa taasisi mbalimbali akizitaka kuchukua tahadhari ili kujikinga na kuwakinga wananchi dhidi ya wimbi la tatu la ugonjwa wa Covid-19.
“Tunawaelekeza wafanyakazi, wanafunzi, ndugu na jamaa wa wagonjwa wote wanaoingia eneo la hospitali kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka yaliyopo katika maeneo mbalimbali ya hospitali au vipukusi (sanitizer),” amesema.
MNH imeelekeza kwa wagonjwa waliolazwa wodini wataruhusiwa kuonwa na ndugu watano tu, ambapo asubuhi wataruhusiwa ndugu wawili, mchana ndugu mmoja na jioni ndugu wawili.