Home FEDHA NI IPI MIPANGO YA FEDHA YAKO?

NI IPI MIPANGO YA FEDHA YAKO?

0 comment 46 views

Je, unajua nini unataka kufanya na fedha zako? Kama bado hufahamu basi tambua kuwa una hatari ya kutumia fedha hizo bila mpangilio. Siku zote kuwa na mpango husaidia kufanikisha mambo makubwa. Ni muhimu kujua kwamba huwezi kutimiza malengo yote uliyonayo na ili kufanikiwa, ni muhimu kuwa na malengo madhubuti ambayo hata ukiwekeza fedha zako, utafaidika.

Ni vyema kukumbuka kuwa, ni rahisi kuweka malengo lakini ni ngumu sana kuyatimiza kwa sababu maneno na matendo ni mambo mawili tofauti. Yafuatayo yanaweza kukusaidia kutambua malengo yako na kuyatimiza:

Jiwekee malengo: Tambua kuwa una mamlaka ya kuweka malengo ya aina yoyote unayotaka ili mradi tu uwe unaamini katika malengo hayo. Ikiwa hujiamini hakuna mtu mwingine atakayekuja kukusaidia kuyaamini malengo hayo na hata kama itatokea, ni mchakato mgumu kwako na kwa wale wanaokusaidia kwani tangu mwanzo hukuwa na imani na malengo hayo. Chukua muda kutafakari mambo ambayo yana umuhimu kwako kisha chagua machache unayoweza kuyafanyia kazi.

Hakikisha una malengo maalum na yanayopimika: Unapoweka malengo yako ni muhimu kuwa na maelezo ya kutosha juu ya yale unayotarajia kutimiza hivyo hakikisha unafafanua haswa maana ya mafanikio katika malengo husika.

Weka malengo yenye busara na maana: Kuweka malengo ambayo unajua kabisa huwezi kufanikisha kutasababisha ushindwe na upoteze muda wako kwa mambo yasiyowezekana. Unapojiwekea malengo maalum, yanayoweza kupimika, hakikisha unaweza kuyafikia malengo hayo. Hivyo unaweza kuwa malengo ambayo yanaweza kuonekana ni madogo lakini utakapoyatimiza, utapata moyo wa kufikia malengo makubwa zaidi.

Gawa malengo: Kutimiza malengo makubwa kunaweza kukatisha tamaa watu wengi kwa sababu ya muda mwingi ambao hutumia. Ili kuendelea kuhamasika kukamilisha malengo yako, gawanya malengo hayo katika mafungu madogo madogo kisha chagua malengo ambayo unaweza kukamilisha kwa wakati unaofaa.

ADVERTISEMENT

Tenga muda: Katika kila lengo unatakiwa kuwa na tarehe ya mwisho ya kukamilisha lengo husika ili kuepuka kutumia muda mwingi katika jambo moja. Kuwa na ratiba kutakuruhusu kufuata mafanikio yako kwa urahisi zaidi na kuhakikisha upo kwenye njia sahihi. Jitahidi kuweka muda usiozidi mwaka ili kujua kila mwaka umefikia wapi na ni lengo gani linatakiwa kupewa kipaumbele zaidi.

Fuatilia maendeleo yako: Mwisho ni muhimu kujua muelekeo wa juhudi zako ili kufikia malengo yako kwa kufanya hivyo itakurahisishia kufanya marekebisho ikiwa yanahitajika. Unaweza kutengeneza jedwali ili kurahisisha ufuatiliaji.

Jiwekee malengo leo na anza kufanikiwa kwa kuyatekeleza. Mawazo pekee hayatoshi hivyo wekeza nguvu na muda wa kutosha ili kutimiza ndoto zako.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter