Serikali kupitia Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imesaini mkataba wa mauzo ya korosho ghafi tani laki moja kwa Kampuni ya ENDO Power Solutions ya Kenya kwa Sh. 418 bilioni. Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Dk. Hussein Mansoor kwa niaba ya serikali ya Tanzania na kwa upande wa Kenya, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ENDO Power Solutions, Brian Mutembei amesaini makubaliano hayo.
Baadhi ya viongozi walioshuhudia zoezi hilo ni Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Innocent Bashungwa, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florence Luoga. Wengine ni Balozi wa Kenya hapa nchini, Dan Kazungu, Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Joseph Buchweshaija, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Prof. Siza Tumbo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Edwin Rutaberuka, Mkurugenzi wa TanTrade, maafisa kutoka serikalini pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumzia hatua hiyo, Prof. Kabudi amempongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wa serikali kununua korosho yote na kuwawezesha wakulima kupata bei inayolingana na jasho lao. Aidha, Waziri Kakunda amewataka watanzania na wamiliki wa viwanda kutokuwa na wasiwasi kwani serikali inalenga kuleta maendeleo kwa wananchi hasa kupitia sekta ya kilimo cha korosho.
“Wakulima wa Korosho wanatakiwa kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi wake ambao unalinda maslahi ya mkulima na umewawezesha kuuza korosho zao kwa faida. Nawakaribisha wafanyabiasha makini kuja nchini kwani Serikali ipo tayari kuwasikiliza watu wa aina hiyo na kufanya nao biashara”. Amesema Kakunda.
Mkataba huo umesainiwa wakati baadhi viongozi hapa nchini wakiwa jijini Arusha kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).