Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tanzania yapiga hatua utakatishaji fedha

Tanzania yapiga hatua utakatishaji fedha

0 comment 105 views

Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi zilizo Mashariki na Kusini mwa Afrika zilizopiga hatua kubwa katika udhibiti wa utakatishaji fedha haramu na uzuiaji wa silaha za maangamizi na ufadhili wa ugaidi.

Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande (Mb), amesema hayo katika Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri na Maafisa Waandamizi wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kudhibiti Utakatishaji Fedha Haramu (Eastern and Southern Africa Anti Money Laundering Group (ESAAMLG), unaofanyika katika mji wa Kasane, nchini Botswana.

Chande amesema Tanzania ipo katika hatua nzuri hasa katika suala zima la kupambana na ugaidi, utakatishaji fedha haramu na uzuiaji wa silaha za maangamizi.

‘’Niwatoe shaka ndugu zangu Watanzania kuwa nchi yetu ipo katika hatua nzuri katika suala zima la kupambana na utakatishaji fedha haramu, ufadhili wa kigaidi pamoja na ufadhili wa silaha za maangamizi’’ ameeleza Chande.

Aidha, amesema Mkutano huo ulitumika kupitia mpango kazi wa Jumuiya ya ESAAMLG na kuangalia ni namna gani wanachama wanaweza kupunguza matumizi ya kuendesha Jumuiya hiyo hasa kwa kuanzisha utaratibu wa kuendesha shughuli za Jumuiya kwa kutumia njia za kieletroniki (Paperless).

Ameongeza kuwa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wamekubaliana kuongeza ajira ya vijana ambao watasaidia katika sekretarieti ya Jumuiya ili kazi za ESAAMLG ziweze kutekelezwa kwa ufanisi zaidi.

Amewataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo za ajira kwa sababu Tanzania ni nchi mojawapo itakayofaidika na ajira hizo na kuongeza kuwa uwepo wa Watanzaia katika Jumuiya utasaidia kujifunza mambo mengi na kupata fursa ya kufaidika kama nchi.

‘’Na imani kubwa kuwa Watanzania wataingia na kuwa sehemu ya ajira hizo na kutakuwa na mafanikio makubwa sana, na uwepo wao ndani ya Jumuiya tutajifunza mengi ambayo yatanufaisha Taifa letu,’’ amesema.

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi wanachama 17.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter